4- Ama Takbiyr tisa juu yake kumepokelewa Hadiyth mbili:

Ya kwanza: ´Abdullaah bin az-Zubayr ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia Hamzah ambapo akampigia Takbiyr tisa… “

Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake na daraja yake katika 02, masuala ya 59, ukurasa wa 82.

Idadi hii ndio ya juu zaidi ambayo tumeiona katika Takbiyr juu ya jeneza. Kwa hiyo watu wakomeke juu yake na wala wasizidishe juu yake. Lakini ana ruhusa ya kupunguza kwenda chini mpaka nne, na ndio idadi ya chini iliopokelewa. Ibn-ul-Qayyim amesema katika “Zaad-ul-Ma´aad” baada ya kutaja baadhi ya mapokezi na Aathaar tulizozitaja:

“Hizi ni Aathaar ambazo ni sahihi. Hakuna kinachopelekea kuzikataa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuzuia kile chenye kuzidi juu ya nne. Bali yeye mwenyewe na Maswahabah zake wamelifanya hilo baada yake.”

Wale wapingaji wametumia hoja juu ya kuzidisha juu ya nne kwa mambo mawili:

Ya kwanza: Maafikiano. Kumekwishatangulia ubainifu wa kosa juu ya hilo.

Ya pili: Yaliyopokelewa katika baadhi ya Hadiyth:

“Yalikuwa ya mwisho katika yale aliyoleta Takbiyr Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nne.”

Jibu: Hii ni Hadiyth dhaifu. Ina njia nyingi lakini hata hivyo baadhi yake zina unyonge zaidi kuliko zengine. Kwa hiyo haitakikani kushikamana nazo kwa kuzirudisha zile zilizothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa cheni za wapokezi Swahiyh na zilizokuja kwa wingi. al-Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw” (05/167) na kabla yake amesema al-Haazimiy katika “al-I´tibaar”, uk. 95 na pia al-Bayhaqiy katika “as-Sunan” (03/74):

“Imepokelewa kwa mitazamo mingi na zote ni dhaifu.”

Kuhusu yaliyotajwa katika “al-Majma´” (03/35):

“Kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalia wale waliouliwa Uhud ambapo akawapigia Takbiyr tisatisa, sabasaba na nnenne mpaka akarudi kwa Allaah.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” na katika “al-Awsatw” kwa cheni ya wapokezi nzuri.”

Hii ni yenye kukataliwa kwa njia mbili:

Ya kwanza: Ni yenye kwenda kinyume na maneno ya al-Haafidhw Ibn Hajar na wale maimamu waliomtangulia ambao wamesema kwa uwazi kwamba njia za Hadiyth zote ni dhaifu.

Ya pili: Hadiyth ameitoa at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (02/120/03) na cheni ya wapokezi wake imekuja ifuatavyo: Ahmad bin al-Qaasim at-Twaa-iy ametuhadithia: Bishr bin al-Waliyd al-Kindiy ametuhadithia: Abu Yuusuf al-Qaadhwiy ametuhadithia: Naafiy´ bin ´Umar ametuhadithia, nimemsikia ´Atwaa´ bin Abiy Rabaah akihadithia kutoka kwa Ibn ´Abbaas kwayo.

Cheni ya wapokezi kama hii haifanywi kuwa nzuri mfano wake. Kwani ndani yake kuna kasoro tatu:

1- Abu Yuusuf al-Qaadhwiy ambaye ni Ya´quub bin Ibraahiym amedhoofishwa na Ibn-ul-Mubaarak na wengineo na al-Fallaas akamsifia kuwa ni mwenye makosa mengi.

2- Unyonge wa Bishr bin al-Waliyd al-Kindiy. Hakika alichanganyikiwa uzeeni.

3- Tofauti ilioko katika cheni ya wapokezi wake. Ameitoa at-Twabaraaniy (01/119/03), al-Haazimiy katika “al-I´tibaar” (95) kutoka kwa wanachuoni waliosema: Kutoka kwa Naafiy´ Abu Hurmuz, kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Ibn ´Abbaas kwayo, mpaka aliposema: “Wale waliouliwa Badr” badala ya “Wale waliouliwa Uhud”.  Hivi ndivo alivoitaja al-Haythamiy na akasema:

“Ndani yake yumo Naafiy´ Abu Hurmuz ambaye ni mnyonge.”

Bali yeye ni mnyonge sana. Ibn Ma´iyn amemtia uongoni. Abu Haatim amesema:

“Ni mwenye kuachwa. Hadiyth ni zenye kwenda na maji.”

Ndiye ugonjwa wa Hadiyth yenyewe. Yeye ndiye amepokea kutoka kwa ´Atwaa´. Yale yaliyotokea katika njia ya kwanza kwamba ni Naafiy´ bin ´Umar – ambaye yeye ni mwaminifu – ni kosa lililitokea kutoka kwa baadhi ya wapokezi wake. Maoni yenye nguvu ni kwamba yeye ni Kindiy ambaye alikuwa amechanganyikiwa uzeeni, kama ulivyokwishatambua.

Ya pili: ´Abdullaah bin ´Abbaas amesimulia:

“Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposimama juu ya mwili wa Hamzah… aliamrisha juu yake akaandaliwa kuelekezwa Qiblah. Kisha akampigia Takbiyr tisa… “

Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 69, Hadiyth ya pili, ukurasa wa 104.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 144-146
  • Imechapishwa: 24/10/2020