74- Atampigia Takbiyr nne, tano mpaka tisa. Yote hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yoyote katika haya atafanya yatasihi. Lakini lililo bora zaidi ni kufanya aina mbalimbali; mara afanye hivi na mara afanye vile. Kama ilivyo shani katika mambo mfano wake kama mfano wa du´aa za kufungulia swalah, matamshi ya Tashahhud na du´aa za Ibraahimiyyah na mfano wake. Ikiwa hakuna budi ila kulazimiana na sampuli moja basi [alete Takbiyr] nne. Kwa sababu juu ya hilo ndio kumepokelewa Hadiyth nyingi. Yafuatayo ni ubainifu wa hayo:

1- Kuhusu Takbiyr nne kumepokelewa Hadiyth kutoka kwa kikosi cha Maswahabah:

Ya kwanza: Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Hadiyth yake imekwishatangulia katika masuala ya 59, 07, kuhusu kumswalia an-Najaashiy na kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpigia Takbiyr nne, ukurasa wa 89.

Ya pili: Kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Imekwishatangulia katika masuala ambayo yameashiriwa katika Hadiyth ya kuhusu kumswalia yule bwana ambaye alizikwa usiku, 06, Hadiyth ya 01, ukurasa wa 87.

Ya tatu: Kutoka kwa Yaziyd bin Thaabit kuhusu swalah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumswalia yule mtumwa wa kike aliyeachwa huru na Banuu fulani katika kaburi lake ambayo iko mahala palipoashiriwa baada ya Hadiyth ya Ibn ´Abbaas.

Ya nne: Kutoka kwa baadhi ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kumswalia kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yule mwanamke masikini kwenye kaburi lake. Hadiyth yake imetajwa mara tu baada ya Hadiyth ya Yaziyd bin Thaabit iliyoashiriwa punde tu.

Ya tano: Abu Umaamah[1] (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Sunnah katika swalah ya jeneza ni kumswalia katika ile Takbiyr ya kwanza mama wa Qur-aan kimyakimya, kisha apige Takbiyr tatu na afanye Tasliym katika ile ya mwisho.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (01/281), Ibn Hazm kutoka kwake (05/129) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kama alivosema al-Haafidhw katika “al-Fath” na an-Nawawiy amemtangulia katika “al-Majmuu´” (05/33) na akazidisha:

“Iko kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

at-Twahaawiy (01/288) amepokea mfano wake na amezidisha mwishoni mwa Hadiyth:

“az-Zuhriy amesema: “Nikakumbuka yale aliyonieleza Abu Umaamah kutokana na hayo juu ya Muhammad bin Suwayd al-Fihriy ambapo akasema kuwa na yeye amemsikia adh-Dhwahhaak bin Qays akihadithia kutoka kwa Habiyb bin Mas-lamah[2] kuhusu swalah ya jeneza mfano wa kile alichokuhadithia Abu Umaamah.”

Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh pia. Iko kwa an-Nasaa´iy. Lakini  adh-Dhwahhaak bin Qays hakuizidisha. Kadhalika ameipokea ash-Shaafi´iy kwa ziada katika matini yake kama itakavokuja katika masuala 79, ukurasa wa 121, 122.

Ya sita: ´Abdullaah bin Abiy Awfa ameeleza:

“Hakika Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipiga Takbiyr nne.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/35) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh katikati ya Hadiyth ambayo itakuja kwa ukamilifu wake katika masuala ya 82.

2- Kuhusu Takbiyr tano ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa ambaye amesema:

“Zayd bin Arqam alikuwa akileta Takbiyr nne juu ya mejeneza yetu. Kuna kipindi alipiga Takbiyr tano juu ya jeneza. Nikamuuliza ambapo akajibu: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizipiga. [Kwa hiyo sintoziacha [kwa yeyote baada yake] abadani].”

Ameipokea Muslim (03/56), Abu Daawuud (02/67, 68), an-Nasaa´iy (01/281), at-Tirmidhiy (02/140), Ibn Maajah (01/458), at-Twahaawiy (01/285), al-Bayhaqiy (04/36), at-Twayaalisiy (674), Ahmad (04/367, 368, 372) kutoka kwake.

Halafu akaitoa at-Twahaawiy na ad-Daaraqutwniy (191, 192), Ahmad (04/370) kupitia njia zengine kutoka kwake mfano wake, ziada ni yao na iliyoko ndani yake ni ya ad-Daaraqutwniy. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Baadhi ya wanachuoni wameliendea hilo katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo. Wameona kuwa Takbiyr juu ya jeneza ni tano. Ahmad na Ishaaq wamesema:

“Imamu akipiga Takbiyr tano juu ya jeneza basi imamu afuatwe.”

3- Ama kuhusu idadi ya Takbiyr sita na saba kumepokelewa juu yake baadhi ya mapokezi yenye kutoka kwa Maswahabah. Lakini hata hivyo ni yenye hukumu ya Hadiyth zenye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baadhi ya Maswahabah wakubwa walizileta juu ya ushuhudio wa Maswahabah wengine pasi na yeyote katika wao kulipinga:

Ya kwanza: ´Abdullaah bin al-Mughaffal ameeleza:

“´Aliy bin Abiy Twaalib alimswalia Sahl bin Hunayf ambapo akampigia Takbiyr sita. Kisha akatugeukia na akasema: “Huyu amehudhuria Badr.”

ash-Sha´biy amesema:

“´Alqamah alifika kutoka Shaam akasema kumwambia Ibn Mas´uud: “Nduguzo Shaam wanayapigia majeneza yao Takbiyr tano. Uzuri ulioje endapo mgelituwekea kikomo tukawa tunakufuateni. ´Abdullaah akakiinamisha kichwa kitambo kidogo kisha akasema: “Yatazameni majeneza yenu na yapigieni Takbiyr kwa mujibu wa vile watavofanya maimamu wenu. Hakuna kikomo wala idadi.”

Ameipokea Ibn Hazm katika “al-Muhallaa” (05/126) kwa ukamilifu wake ambaye amesema:

“Hii cheni ya wapokezi iko katika kilele katika usahihi.”

Abu Daawuud katika “al-Masaa-il” yake amepokea kutoka kwake kisa cha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Imaam Ahmad, uk. 152, at-Twahaawiy (01/287), al-Haakim (03/409), al-Bayhaqiy (04/36) na cheni za wapokezi wao ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Iko kwa al-Bukhaariy katika “al-Maghaaziy” (07/253) pasi na maneno “sita… “

Kisa cha Ibn Mas´uud amekitoa at-Twahaawiy na al-Bayhaqiy (04/37) mfano wake.

Ya pili: ´Abd Khayr amesimulia:

“´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akiwapigia Takbiyr sita wale waliohudhuria vita vya Badr, Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tano na watu wengine nne.”

Ameipokea at-Twahaawiy na ad-Daaraqutwniy (191) na al-Bayhaqiy kupitia njia yake (04/37). Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh na wapokezi wake wote ni waaminifu.

Ya tatu: Muusa bin ´Abdillaah bin Yaziyd ameeleza:

“´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimswalia Abu Qataadah na akampigia Takbiyr saba. Alikuwa ni katika wale waliohudhuria Badr.”

Ameipokea at-Twahaawiy na al-Bayhaqiy (04/36) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Lakini al-Bayhaqiy ameitia kasoro kwa kusema:

“Ni kosa. Kwa sababu Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) alibakia baada ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kwa muda mrefu.”

al-Haafidhw katika “at-Talkhiysw” (1665) akamrudi kwa kusema:

“Nasema: “Kasoro hii si yenye kutia dosari. Kwa sababu pia imesemekana kuwa Abu Qataadah alikufa katika uongozi wa ´Aliy, jambo ambalo ndilo lenye nguvu.”

Ibn-ut-Turkumaaniy amemtangulia katika hilo katika “al-Jawhar-un-Naqiyy”. Kirejee!

Mapokezi haya ni Swahiyh kutoka kwa Maswahabah ni Swahiyh ambayo yanajulisha kuwa kuyatendea kazi hayo kwa tano na sita ni jambo lililoendelea mpaka baada ya kuondoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo ni kinyume na yale waliyodai maafikiano ya wanachuoni juu ya Takbiyr nne peke yake. Ibn Hazm amehakiki kauli juu ya ubatilifu wa madai hayo katika “al-Muhallaa” (05/124-125).

[1] Huyu si yule Abu Umaamah al-Baahiliy ambaye ni yule Swahabah anayetambulika. Huyu ni mwengine ambaye pia ni maarufu kwa kunyah yake. Jina lake ni As´ad. Imesemekana vilevile kwamba ni Sa´d bin Sa´d bin Haniyf al-Answaariy ambaye anahesabika ni katika Maswahabah. Alipata maono lakini hakusikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hiyo Hadiyth ni katika Maraasil za Swahabah, ambayo ni hoja.

[2] Ni Habiyb bin Mas-lamah bin Maalik al-Fahriy al-Makkiy. Alikuwa akiitwa Habiyb ar-Ruum kwa sababu ya wingi wa kuwaingilia kwao hali ya kuwa ni mpiganaji jihaad. Kuna tofauti juu ya uswahabah wake. al-Haafidhw amesema:

”Maoni yenye nguvu ni kuthibiti kwake. Lakini hata hivyo alikuwa mdogo.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 141-144
  • Imechapishwa: 14/10/2020