72. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya mpangilio wa ubora wa Maswahabah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na kwamba mbora wa Ummah wake ni Abu Bakr as-Swiddiyq, kisha ´Umar al-Faaruq, kisha ´Uthmaan Dhun-Nuurayn, kisha ´Aliy al-Murtadhwaa, kisha wale kumi waliobakia, halafu waliopigana vita vya Badr, kisha waliokula kiapo chini ya mti halafu Maswahabah wengine waliobaki – Allaah amewawia radhi nao wamemuia radhi.

MAELEZO

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ndio watu bora wa Ummah huu na waislamu bora kabisa na hakuna yeyote anayelingana nao. Hayo ni kwa sababu ya kupwekeka kwao na sifa ya kusuhubiana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kupambana jihaad bega kwa bega pamoja nao na kupokea elimu kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wana sifa maalum ambazo waumini wengine hawana. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wenu ni karne yangu, kisha wale wataofuatia, kisha wale wataofuatia.”[1]

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau mmoja wenu atatoa dhahabu kiasi cha mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vilivyojazwa na mikono vya mmoja wao wala nusu yake.”[2]

Amekataza kuwatukana Maswahabah zake, kuwaponda na kuwachukia. Halafu akabainisha fadhilah zao na kwamba matendo yao ni bora kuliko matendo ya wengine. Tuchukulie mfano wa swadaqah. Kwa mfano mtu atajitolea swadaqah mfano wa mlima wa Uhud kwa ajili ya Allaah basi haitofikia Mudd ambayo ni robo ya Swaa´ iliyotolewa na mmoja katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili ni kutokana na fadhilah zao (Radhiya Allaahu ´anhum) na nafasi yao. Kitendo kinalipwa maradufu kutokana na utukufu wa mtendaji mbele ya Allaah (Ta´ala). Wao ndio karne bora ya Ummah huu bila kipingamizi.

Ni lazima kuwapenda, kuwatukuza, kuwaheshimu na kutompunguza yeyote katika wao. Wala haifai kuingia ndani ya yale yaliyopitika kati yao kipindi cha fitina. Wala haijuzu kumtia mmoja katika makosa na kumtia mwingine katika usawa katika Maswahabah. Kwa sababu wote ni Mujtahiduun. Haijuzu kupekua makosa yao na kusema fulani alifanya kitu fulani na mwingine amefanya kitu fulani kutokana na fadhilah zinazofunika makosa yao – yakiwepo kweli. Likipatikana jambo kutoka kwa mmoja wao basi ana lukuki ya fadhilah zinazofunika makosa haya (Radhiya Allaahu ´anhum).

Swahabah mmojammoja hakukingwa na makosa. Kosa linaweza kutokea kutoka kwa mmojammoja katika wao. Lakini wana fadhilah tele zinazofunika kosa hili. Kuhusu maafikiano yao ni wenye kulindwa kwayo. Maswahabah ni wenye kulindwa kwa mkusanyiko wao.

[1] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535) kupitia kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] al-Bukhaariy (3273) na Muslim (2541) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh). Ameipokea vilevile Muslim (2540) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 101-103
  • Imechapishwa: 18/05/2021