Hesabu maana yake kilugha ni kuhesabu. Hesabu maana yake katika Shari´ah ni Allaah kuwaonyesha waja matendo yao. Ni kitu kimethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na kwa maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم 

“Hakika ni Kwetu marejeo yao, kisha bila shaka ni juu Yetu hesabu yao.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika baadhi ya swalah zake:

اللهم حاسبني حسابًا يسيرًا

“Ee Allaah! Nifanyie hesabu nyepesi.”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) akasema: “Ni ipi hesabu nyepesi?” Akasema: “Ni kule kukitazama kitabu chake kisha akamsamehe.”

Ameipokea Ahmad. al-Albaaniy amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.”[2]

Waislamu wameafikiana juu ya kuthibiti kwa hesabu siku ya Qiyaamah.

Namna ambavyo muumini atafanyiwa hesabu ni kwamba Allaah atamweka chemba na kumkariria dhambi zake mpaka pale atakapoona kuwa ameangamia ndipo Allaah atamwambia: “Nimekusitiri duniani na Mimi hii leo nakusamehe.” Ndipo apewe daftari la matendo yake. Kuhusu makafiri na wanafiki wataitwa kwa sauti juu ya vichwa vya viumbe: “Watu hawa ndio ambao wamemkadhibisha Mola wao. Laana ya Allaah iwe juu ya madhalimu.”[3]

Kuna maafikiano juu yake kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Umar.

Hesabu ni yenye kuwaenea watu wote isipokuwa wale wataobaguliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nao ni wale watu 70.000 kutoka katika Ummah huu, ikiwa ni pamoja vilevile na ´Ukkaashah bin Muhswin, ambao wataingia Peponi bila ya hesabu wala adhabu.”

Kuna maafikiano juu yake.

Ahmad amepokea kupitia kwa Thawbaan ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pamoja na kila mmoja atakuwa pamoja na 70.000 wengine.”[4]

Ibn Kathiyr amesema.

“Hadiyth hii ni Swahiyh na akaitajia Hadiyth nyingine zenye kuitia nguvu.”[5]

[1] 88:25-26

[2] Ameipokea Ahmad (06/48), Ibn Abiy ´Aaswim katika kitabu ”as-Sunnah” (885) na tamko ni la Ahmad. al-Albaaniy amesema katika ”Takhriyj-us-Sunnah” (02/429):

”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

Msingi wa Hadiyth hii iko kwa al-Bukhaariy (103, 6536, 6537) na Muslim (2876, 79).

[3] al-Bukhaariy (2441) na Muslim (2768, 52).

[4] al-Bukhaariy (6541) na Muslim (220, 374).

[5] at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr” (05/280, 281).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 117-118
  • Imechapishwa: 29/11/2022