Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Watafufuliwa watu siku ya Qiyaamah wakiwa uchi, peku na bila ya kutahiriwa. Watasimama katika kisimamo cha siku ya Qiyaamah mpaka pale ambapo Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awashufaie. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atawafanyia hesabu, itapimwa mizani na vitabu vya mateno vitagawanywa kwa mkono wa kulia na wa kushoto:

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًاوَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِفَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًاوَيَصْلَىٰ سَعِيرًا

”Ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, basi atahesabiwa hesabu nyepesi na atageuka kwa ahli zake hali ya kuwa ni mwenye furaha. Na ama yule atakayepewa kitabu chake nyuma ya mgongo wake, basi ataomba maangamizi na ataingia aungue Moto uwakao.”[1]

MAELEZO

Kufufuliwa maana yake kilugha ni kupelekwa na kukusanywa. Kufufuliwa maana yake katika Shari´ah ni kuwafufua wafu siku ya Qiyaamah.

Kukusanywa maana yake kilugha ni kukusanya. Kukusanywa maana yake katika Shari´ah ni kuwakusanya viumbe siku ya Qiyaamah ili kuwafanyia hesabu na kuhukumu kati yao.

Kufufuliwa na kukusanywa ni jambo la haki lililothibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala):

قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ

“Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa.”[2]

قُلْ إِنَّ الْأَوَّلِينَ وَالْآخِرِينَ لَمَجْمُوعُونَ إِلَىٰ مِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ 

”Sema: ”Hakika wa awali na wa mwishoni, bila shaka wote watakusanywa katika wakati na mahali siku maalum.””[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watakusanywa siku ya Qiyaamah katika ardhi nyeupe wekundu kama kipande cha unga kilicho safi. Hakuna humo alama ya yeyote.”[4]

Kuna maafikiano juu yake.

Waislamu wameafikiana juu ya kuthibiti kukusanywa siku ya Qiyaamah.

Watu watakusanywa hali ya kuwa hawana viatu, uchi pasi na mavazi na bila kutahiriwa. Amesema (Ta´ala):

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ

“Kama Tulivyoanza uumbaji umbo la mwanzo tutalirudisha. Hiyo ni ahadi juu Yetu.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika nyinyi mtafufuliwa hali ya kuwa hamna viatu, uchi na pasi na kutahiriwa.” Kisha akasoma:

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ

“Kama Tulivyoanza uumbaji umbo la mwanzo tutalirudisha. Hiyo ni ahadi juu Yetu – hakika sisi ni wafanyao.”[6]

Wa kwanza atakayevishwa nguo ni Ibraahiym.”

Kuna maafikiano juu yake.

Vilevile katika Hadiyth ya ´Abdullaah bin Unays iliyopokelewa na Ahmad ambaye amesimulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Watu watakusanywa siku ya Qiyaamah hali ya kuwa uchi, pasi na kutahiriwa na pasi na kuwa na chochote.”

[1] 84:7-12

[2] 64:07

[3] 56:49-50

[4] al-Bukhaariy (6521) na Muslim (2790, 28).

[5] 21:104

[6] 21:104

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 114-116
  • Imechapishwa: 29/11/2022