Kupulizwa ni kitu kinatambulika. Parapanda maana yake kilugha ni pembe. Parapanda maana yake katika Shari´ah ni pembe ambayo ameifunga Israafiyl mdomoni mwake anasubiri ni lini ataamrishwa kuipuliza.

Israafiyl ni mmoja katika Malaika watukufu ambao wanabeba ´Arshi. Ni mapulizo mawili:

1 – Upuzio wa kufazaika. Atapuliza ndani yake ambapo wafazaike na kuzimia watu isipokuwa wale atakaotaka Allaah.

2 – Upuzio wa kufufuka. Atapuliza ndani yake ambapo wasimame na wafufuke kutoka ndani ya makaburi yao.

Kupulizwa parapanda ni jambo limefahamishwa na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Ummah. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ

“Itapulizwa katika baragumu, basi watazimia wale walioko mbinguni na ardhini isipokua amtakaye Allaah. Kisha litapulizwa humo jengine, tahamaki hao wanasimama wakitazama.”[1]

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ

“Litapulizwa baragumu, basi tahamaki wanatoka makaburini mwao wakienda mbiombio kwa Mola wao.”[2]

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kisha kutapulizwa parapanda na hakuna yeyote atakayeisikia isipokuwa atainamisha shingo yake na kuinua mara nyingine shingo yake. Kisha hatobakia yeyote isipokuwa atafariki. Halafu Allaah atateremsha mvua kana kwamba ni mvua nyepesi ambapo itamea miili ya watu. Kisha kutapulizwa parapanda nyingine na tahamaki watasimama na huku wanaangalia.”

Ameipokea Muslim katika Hadiyth ndefu.

Ummah umeafikiana juu ya kuthibiti kwake.

[1] 39:68

[2] 36:51

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 114
  • Imechapishwa: 29/11/2022