70. Wanawake ambao wanafaa kutazama viungo visivyotakiwa vya mwanamke wa Kiislamu

Kuna kidokezo muhimu maana ya maneno Yake Allaah (Ta´ala):

أَوْ نِسَائِهِنَّ

”… au wanawake wao… ”[1]

Bi maana waumini wanawake, kama alivosema Mujaahid na wengine katika Salaf, na si wanawake wema pasi na kujali dini yao, kama walivosema baadhi hii leo. ash-Shawkaaniy amesema:

”Wanawake kuegemezwa kwao kunafahamisha kuwa inawahusu waumini wa kike peke yao.”[2]

al-Bayhaqiy amesema:

”Ama kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

أَوْ نِسَائِهِنَّ

”… au wanawake wao… ”

tumesimuliwa ya kwamba ´Umar bin al-Khattwaab alimwandikia Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah: ”Wanawake wa Kiislamu wanaoingia bafu za nje pamoja na wanawake katika watu wa Kitabu; wazuie wasiingie.”

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho, kutazama uchi wake isipokuwa watu wanaochangia imani naye.”[3]

Upokezi wa kwanza kwa al-Bayhaqiy ameupokea al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan” kupitia kwa ´Iysaa bin Yuunus: Hishaam bin al-Ghaaz bin Rabiy´ah al-Jarshiy ametuhadithia, kutoka kwa ´Ubaadah bin Nusay al-Kindiy. Ameipokea Ibn Jariyr pia. Wapokezi wake ni wenye kuaminika, lakini cheni yake ya wapokezi imekatika kwa sababu ´Ubaadah hakuwahi kukutana na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Kati yao yuko Nusay, ambaye ni baba yake na ´Ubaadah. Ibn Kathiyr ametaja katika tafsiri yake ya Qur-aan kwamba Sa´iyd bin Mansuur ameipokea katika ”as-Sunan” yake, na kupitia kwake al-Bayhaqiy: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa Hishaam bin al-Ghaaz, kutoka kwa ´Ubaadah bin Nusay, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa al-Haarith bin Qays. Wapokezi wake wote ni wenye kuaminika – isipokuwa Nusay. Hakuna mwingine isipokuwa tu Ibn Hibbaan ndiye kamzingatia kuwa ni mwenye kuaminika[4]. Haafidhw Ibn Hadjar amesema juu yake ”at-Taqriyb”:

”Hatambuliki.”

Hata hivyo wafasiri na wahakiki, kama vile Ibn Jariyr, Ibn Kathiyr, ash-Shawkaaniy na wengineo, wameafikiana juu ya maana yake. Maana yake haitoki nje ya tafsiri iliyopokelewa na haizingatii maoni ya wale waliokuja nyuma.

[1] 24:31

[2] Fath-ul-Qadiyr (4/22).

[3] Kitaab-ul-Adab, uk. 407

[4] ath-Thiqaat (5/482).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 115-116
  • Imechapishwa: 09/10/2023