Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kushoto juu ya goti la kushoto, akikunja vidole vyake vyote vya mkono wa kulia na huku akiashiria kidole cha shahadah kuelekea Qiblah na akikitazama[1].

Alikuwa anapoashiria kwa kidole chake cha shahadah huweka kidole chake cha gumba juu ya kidole cha katikati[2]. Wakati mwingine alikuwa anaweza kufanya vidole viwili hivyo kama duara[3].

Alipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akinyanyua kidole chake cha shahadah anakitikisa na huku akiomba du´aa[4].

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika ni kikali zaidi dhidi ya shaytwaan kuliko chuma.”[5]

Bi maana kidole cha shahadah.

Maswahabah wa Mtume (Swalla ´alayhi wa sallam) walikuwa wakikumbushana juu ya kuashiria kidole cha shahadah wakati wa kuomba du´aa[6].

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifanya hivo katika Tashahhud zote[7].

Alimwona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu ambaye anatikisa kidole chake na huku anaomba du´aa ambapo akasema:

“Moja! Moja!”

na akaashiria kidole cha shahadah[8].

[1] Muslim, Abu ´Awaanah na Ibn Khuzaymah. al-Humaydiy amezidisha katika “al-Musnad” yake (01/131) na kadhalika Abu Ya´laa amefanya hivo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Ibn ´Umar:

“Ni pigo kwa shaytwaan. Haitakikani kwa mtu kusahau kufanya hivo.”

al-Humaydiy akanyanyua kidole chake. al-Humaydiy amesema:

“Muslim bin Abiy Maryam amesema: “Kuna mtu alinieleza kwamba aliona picha za Mitume kwenye kanisa huko Shaam wakifanya hivo katika swalah zao” na akanyanyua kidole chake.

Hii ni faida ya kipekee na maalum. Cheni ya wapokezi kwa mtu huyu ni Swahiyh.

[2] Muslim na Abu ´Awaanah.

[3] Abu Daawuud, an-Nasaa’iy, Ibn-ul-Jaaruud katika ”al-Muntaqaa” (208), Ibn Khuzaymah (1/86/1-2) na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” (485). Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Ibn-ul-Mulaqqin ameisahihisha (2/28). Ibn ´Adiyy (1/287) amepokea Hadiyth inayotolea ushahidi juu ya kutikisa kidole. Amesema kuhusu mpokezi wake ´Uthmaan bin Muqsim:

“Ni dhaifu, lakini hata hivyo Hadiyth zake zinaweza kuandikwa.”

Kuhusiana na Hadiyth “Alipokuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akinyanyua kidole chake cha shahadah anakitikisa na huku akiomba du´aa” at-Twahaawiy amesema:

“Hapa kuna dalili inayofahamisha kwamba ilikuwa mwishoni mwa swalah.”

Ni dalili inayofahamisha kwamba Sunnah ni kuendelea kuashiria kidole na kukitikisa mpaka wakati wa Tasliym kwa sababu du´aa inakuwa kabla ya Tasliym. Haya ndio maoni ya Maalik na wengineo. Ahmad aliulizwa kama mtu aashirie kidole chake wakati wa swalah ambapo akajibu:

“Ndio, tena kwa nguvu.” (Masaa-il-ul-Imaam Ahmad, uk. 80, ya Ibn Haaniy’)

Ni dalili inayothibitisha kwamba kuashiria kwa kidole ni Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ahmad na maimamu wengineo wa Ahl-us-Sunnah waliitendea kazi. Hivyo wamche Allaah wale wanaosema kwamba kitendo kama hicho hakina maana yoyote na hakisilihi ndani ya swalah. Kwa ajili hiyo wao hawatikisi pamoja na kujua kwao kwamba kitendo hichi kimethibiti. Wanajaribu kupindisha kwa njia ambayo haiendani kabisa na usulubu wa kiarabu na uelewa wa maimamu.

Lililo la ajabu ni kwamba baadhi yao wanamtetea imamu katika masuala mengine mbali na haya – japokuwa maoni yake yatakuwa yanapingana na Sunnah –  kwa hoja kwamba kusema kuwa amekosea ni kumkosea adabu. Halafu wanaisahau na kuirudisha Sunnah hii iliyothibiti na kuwadharau wale wenye kuitendea kazi. Kwa kujua – au pasi na kujua – dharua zao zinawagusa maimamu hawa ambao mara nyingi huwatetea kwa batili. Wao katika maudhui haya wamepatia Sunnah. Bali uhakika wa mambo ni kwamba dharau zao zinamgusa mpaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu yeye ndiye aliyekuja nalo. Kwa hivyo kuwadharau wao ni kumdharau yeye:

فَمَا جَزَاءُ مَن يَفْعَلُ ذَٰلِكَ مِنكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَىٰ أَشَدِّ الْعَذَابِ

“Hapana malipo ya anayefanya hayo miongoni mwenu isipokuwa ni utwevu katika maisha ya dunia na siku ya Qiyaamah watapelekwa katika adhabu kali zaidi.” (02:85)

Ama kuashiria kidole cha shahaadah kwa juu wakati wa kukanusha na kuashiria kwa chini wakati wa kuthibitisha ni jambo lisilolokuwa na msingi katika Sunnah. Kutokana na inavyofahamisha Hadiyth ni jambo linalopingana na Sunnah.

Ama kuhusu Hadiyth isemayo “Usikitikise” mlolongo wa wapokezi wake haukuthibiti, kama nilivyobainisha katika “Dhwa´iy Abiy Daawuud” (175). Hata kama ingekuwa imethibiti basi imekuja kwa njia ya kukanusha na Hadiyth ya mlango huu imekuja kwa njia ya kuthibitisha. Uthibitishaji unatangulia mbele ya ukanushaji, kama inavyotambulika kwa wanachuoni. Kwa hivyo hakuna dalili kwa wale wanaopinga kutikiswa kwa kidole.

[4] Tazama maelezo yaliyotangulia.

[5] Ahmad, al-Bazzaar, Abu Ja´far, al-Bakhtariy katika ”al-Amaaliy” (1/60), at-Twabaraaniy katika ”ad-Du´aa’” (1/73), ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy katika ”as-Sunan” (2/12) kwa cheni ya wapokezi nzuri, ar-Rawayyaaniy katika ”al-Musnad” (2/249) na al-Bayhaqiy.

[6] Ibn Abiy Shaybah (2/123/2) kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri.

[7] an-Nasaa’iy na al-Bayhaqiy kwa cheni ya wapokezi ilio nzuri.

[8] Ibn Abiy Shaybah (1/40/12) na (2/123/2) na an-Nasaa’iy. al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Ina uppokezi wenye kuitilia nguvu kwa Abiy Shaybah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 137-139
  • Imechapishwa: 30/12/2018