70. Kichenguzi cha pili cha swawm: Kutokwa na manii

2 – Mtu kutoa manii kwa khiyari yake kwa kubusu, kupapasapapasa, punyeto au njia zingine. Kwa sababu mambo hayo ni katika matamanio ambayo swawm haisihi isipokuwa kwa kujiepusha nayo, kama ilivyopokelewa katika Hadiyth-ul-Qudsiy:

“Anaacha chakula chake, kinywaji chake na matamanio yake kwa ajili Yangu.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Kuhusu kubusu na kupapasapapasa pasi na kutokwa na manii hakufunguzi. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akibusu hali ya kuwa amefunga, lakini alikuwa ni mwenye kuweza kujizuia vyema kuliko nyinyi.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kuwa ´Umar bin Abiy Salamah alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, mfungaji abusu?” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Muulizeni huyu – bi maana Umm Salamah – ambapo akamweleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivo.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba mimi ndiye ninayemcha Allaah zaidi kuliko nyinyi na mwenye kumukhofu zaidi.”

Lakini ikiwa mfungaji anachelea juu ya nafsi yake kutokwa na manii kwa kubusu na mengineyo au yakampelekea hatua kwa hatua mpaka akafanya jimaa kwa sababu ya kutokuwa na nguvu ya kuzuia matamanio yake, basi katika hali hiyo itakuwa ni haramu kubusu na mfano wake kwa ajili ya kuziba njia na kuilinda swawm yake kutokana na vinavyoiharibu. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwamrisha anayetawadha kufanya kishindo katika kupandisha maji puani isipokuwa akiwa ni mfungaji kwa kuchelea maji yasiingie tumboni mwake.

Ama kutokwa na manii usingizini au kwa kufikiria tu kitendo chenyewe hakumfunguzi mtu. Kwa sababu kuota hakutokani na khiyari ya mfungaji. Kuhusu kufikiria ni jambo lenye kusamehewa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ameusamehe ummah wangu yale yanayonong´onezwa na nafsi zao muda wa kuwa hawajayatenda au kuyafanya.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 98-99
  • Imechapishwa: 22/02/2024