Allaah (Ta´ala) amesema:

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Katika Aayah hii tukufu Allaah ametaja misingi ya vifunguzi vya swawm na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallm) katika Sunnah akataja ukamilifu wa vitu hivyo. Kuna vifunguzi aina saba:

1 – Jimaa ikiwa na maana ya kuingiza dhakari ndani ya uke, kitu ambacho ni khatari na dhambi yake ni kubwa zaidi. Pale ambapo mfungaji atakapojamii basi swawm yake inachenguka. Ni mamoja swawm hiyo ni ya faradhi au inayopendeza. Isitoshe ikiwa ni mchana wa Ramadhaan na swawm hiyo inamuwajibikia basi atalazimika pia, mbali na kulipa siku hiyo, kutoa kafara kubwa; kuacha huru mtumwa muumini, asipoweza basi atafunga miezi miwili mfululizo. Hatoruhusu kukatisha isipokuwa kwa udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah, kama vile masiku ya ´iyd au masiku ya Tashriyq, au udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah, kama vile maradhi au safari iliyopangwa kwa lengo lisilokuwa la kufungua. Akila pasi na udhuru, ijapo ni siku moja tu, basi atalazimika kuanza swawm upya ili kupatikane kule kufuatanisha. Asipoweza kufunga miezi miwili mfululizo basi atawalisha masikini sitini ambapo kila masikini atampa nusu kilo na gramu kumi za ngano nzuri[2]. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kuhusu bwana mmoja aliyemwingilia mke wake katika Ramadhaan ambapo akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu hilo ambapo akamuuliza:

“Je, unaweza kupata mtumwa?” Akajibu: “Hapana.” Akamuuliza: “Je, unaweza kufunga miezi miwili?” Akikusudia kwa kufululiza, kama ilivyopokelewa katika mapokezi mengine. Bwana yule akajibu: “Hapana.” Akamuuliza: “Lisha masikini sitini.”

Hadiyth hii imepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kwa ukamilifu wake.

[1] 02:187

[2] Inasihi pia kutoa mchele badala ya ngano. Lakini mtu anatakiwa azingatie uzito; ikiwa mchele ndio mzito zaidi basi kutaongezwa uzito wake kwa kipimo chake, na ikiwa ndio mwepesi basi kutapunguzwa uzito wake kwa kipimo chake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 98
  • Imechapishwa: 21/02/2024