Waja wa Allaah! Hiki hapa Kitabu cha Allaah kinachosomwa na kusikizwa mbele yenu. Nayo ni Qur-aan ambayo endapo ingeliteremshwa juu ya majibali basi mgeliiona ni yenye kuogopa na kusambuka. Pamoja na haya hakuna sikio lenye kusikia, jicho lenye kutokwa na machozi, moyo wenye kuogopa wala utekelezaji wa Qur-aan mtu akatarajia kuwa itamfanyia mtu maombezi. Nyoyo zimekosa uchaji na zimeharibika na zimepiga giza la madhambi ambapo zimekuwa hazioni wala hazisikii. Ni mara ngapi tunasomewa Aayah za Qur-aan na nyoyo zetu zimekuwa kama mawe bali ngumu zaidi! Ni mara ngapi tunapitiwa na mwezi wa Ramadhaan na hali zetu ndani yake ni kama hali za wala maangamivu! Hakuna kijana katika sisi ambaye anakoma kutokama na ujana wala mtumzima anayekoma kutokamana na maovu ambapo akaungana na wema. Sisi tuko wapi na wale watu ambao pindi wanaposikia mlinganizi wa Allaah basi huitikia ulinganizi wake na anaposomewa Aayah Zake basi moyo wake unatikisika kwelikweli. Hao ni watu ambao wameneemeshwa na Allaah ambapo wakatambua haki Yake na wakagua salama kwao.

Ibn Mas´uud amesema:

“Msomaji wa Qur-aan anatakiwa utambulike usiku wake pindi watu wamelala, mchana wake pindi watu wanakula, machozi yake pindi watu wanacheka, kujichunga kwake pindi watu wanapojiachia hovyo, kunyamaza kwake pindi watu wanapokurupuka, unyenyekevu wake pindi watu wanapovuruga na huzuni wake pindi watu wanapofurahi.”

Ndugu wapendwa! Ihifadhini Qur-aan kabla ya kupitwa na fursa. Ihifadhini mipaka yake kutokamana na kuzembea na kuasi. Tambueni kuwa itakuwa ni yenye kutoa ushahidi juu yenu au dhidi yenu mbele ya Allaah. Sio kuishukuru neema ya Allaah kwa kuiteremsha sisi tukaiweka nyuma ya migongo yetu. Pia sio katika kuadhimisha matukufu ya Allaah kuzichezea shere hukumu za Allaah:

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي ۗ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا

“Na siku dhalimu atakapouma mikono yake akisema: “Laiti ningeshika njia pamoja na Mtume. Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani; kwani hakika amenipoteza na Ukumbusho baada ya kunijilia. Na shaytwaan kwa binadamu daima ni msaliti. Na Mtume akasema: “Ee Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan yenye kuhamwa. Na hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wahalifu. Na Mola wako Anatosheleza kuwa ni Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.”[1]

[1] 25:27-31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 87-88
  • Imechapishwa: 21/02/2024