71- Inafaa kuliswalia jeneza msikitini. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Siku alipoifariki Sa´d bin Abiy Waqqaas wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walituma ujumbe wao kwamba waliingize msikitini ili wapate kuliswalia. Likasimamishwa katika vyumba vyao ambapo wakamswalia. Lilitolewa kutokea mlango wa majeneza uliokuwa katika maqaaid. Wakafikiwa na khabari kwamba wapo watu waliolitia dosari jambo hilo na wakasema: [“Hii ni Bid´ah.] Haijawahi kutokea majeneza kuingizwa msikitini. Hayo yakamfikia ´Aaishah ambapo akasema: “Ni pupa iliyoje walionayo watu mpaka wakaweza kuishi katika kuyazungumza yale wasiyokuwa na elimu nayo! Wametutia dosari kwa kulipitisha jeneza msikitini. Ninaapa kwa Allaah kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumswalia Suhayl bin Baydhwaa´ [na nduguye] isipokuwa ndani ya msikiti.”

Ameipokea Muslim (03/63) kupitia njia mbili kutoka kwake na watunzi wa Sunan na wengineo. Pia nimeitoa katika “Ahkaam-ul-Masaajid” kutoka katika kitabu changu “ath-Thamarah al-Mustatwaab”. Ziada ni za Muslim isipokuwa ya kwanza ambayo ni ya al-Bayhaqiy (04/51).

72- Lakini bora ni kuliswalia nje ya msikiti mahali palipoandaliwa kuyaswalia majeneza. Hivo ndivo lilivokuwa jambo katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ndivo uongofu wake alivokuwa akifanya mara nyingi. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

Ya kwanza: Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Hakika mayahudi walikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakiwa na bwana mmoja katika wao na mwanamke aliyezini ambapo akaamrisha wakapigwa mawe karibu na maeneo ya majeneza karibu na msikiti.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy (04/155) na ameifanyia kichwa cha khabari na Hadiyth ya nne kwa “Mlango unaozungumzia swalah ya jeneza uwanja mahala pa kuswalia na msikitini”.

Ya pili: Jaabir ameeleza:

“Kuna bwana mmoja katika sisi alifariki ambapo tukamwosha… tukamweka kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mahala yanapowekwa majeneza sehemu ya Jibriyl. Kisha tukamjuza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili amswalie. Akaja pamoja nasi… akamswalia… “

 Ameipokea al-Haakim na wengineo. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 17, Hadiyth ya tatu, nambari 11 ukurasa wa 16.

Kuhusiana na masuala haya kumepokelewa Hadiyth kutoka kwa baadhi ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth yake imekwishapita katika masuala 59, Hadiyth ya 4 katika kipengele cha sita, ukurasa wa 89.

Ya tatu: Muhammad bin ´Abdillaah bin Jahsh amesimulia:

“Tulikuwa tumekaa katika uwanja wa msikiti mahala yanapowekwa majeneza ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekaa kati yetu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akainua macho yake kutazama juu ya mbinguni… “

Ameitoa Ahmad (05/289) na al-Haakim (02/24) ambaye amesema:

“Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye katika “Talkhiysw” na al-Mundhiriy akamkubalia katika “at-Targhiyb” (03/34). Ndani yake yuko Abu Kathiyr, ambaye ni mtumwa aliyeachwa huru na Muhammad bin Jahsh. Ibn Abiy Haatim amemtaja (04/02/429, 430) na hakutaja juu yake kumjeruhi wala kumsifu. Vivyo hivyo ndivo alivosema al-Haythamiy katika “al-Majma´” (04/127): “Amesitiriwa”. Pia amemtaja Ibn Hibbaan katika “ath-Thiqaat” (05/570). Pamoja na hayo al-Haafidhw amesema juu yake katika “at-Taqriyb”: “Mwaminifu” na akataja katika “at-Tahdhiyb” kwamba wako waaminifu wengi waliopokea kutoka kwake na kwamba alizaliwa katika zama za uhai wake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu kama huyu Hadiyth yake inakuwa nzuri – Allaah (Ta´ala) akitaka – na khaswa ikiwa ni katika zile shawahidi.

Ya nne: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Kwaamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitangaza kuhusu kifo cha an-Najaashiy katika ile siku aliyokufa. Akatoka kwenda mahala pa kuswalia, akawapanga safu na kupiga Takbiyr nne.”

Wameipokea al-Bukhaariy na Muslim na wengineo kwa matamshi na ziada nyingi. Tumekwishatangulia kuitaja kwa pamoja katika mtiririko mmoja pamoja na ziada nyenginezo katika Hadiyth za Maswahabah wengine. Nimeyabainisha hayo katika masuala ya 59, Hadiyth ya 7, ukurasa wa 89-90.

al-Bukhaariy ameiwekea kichwa cha khabari Hadiyth hii kutokana na yale yanayojulisha ambayo ni kuswali mahali pa kuswalia, kama ilivyotangulia kutajwa katika Hadiyth ya kwanza.

Miongoni mwa mambo yanayoshangaza ni ule msimamo wa al-Haafidhw na al-Bayhaqiy juu ya Sunnah hii – nikimaanisha kuyaswalia majeneza mahala au uwanja wa kuswalia (Muswallaa) – Kwani hakika yeye masuala haya hajayawekea mlango maalum katika kitabu chake “as-Sunan al-Kubraa” pamoja na kwamba zipo Hadiyth nyingi zilizopokelewa juu ya jambo hili, kama ulivyoona. Pamoja na kwamba yeye ameweka mlango wa kujitegemea juu ya kuliswalia jeneza ndani ya msikiti licha ya kuwa suala hilo halina zaidi ya Hadiyth ya ´Aaishah. Kisha wakapita juu ya mwenendo wake baadhi Shaafi´iyyah katika vitabu vyao vifupi ambapo wakaghafilika kuyaswalia majeneza katika mahala pa kuswalia. Mfano wa watu hao ni an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) katika “Minhaaj-ut-Twaalibiyn” (Makhtuta 34-02) ambapo amesema:

“Inafaa kumswalia [maiti] msikitini.”

Endapo katika maneno yake angeongezea:

“Pia imesuniwa kuliswalia [jeneza] mahapa la kuswalia.”

basi angelikuwa amepatia zaidi.

al-Baajuuriy katika “Haashiyah ´alaa Ibn-il-Qaasim” (01/424) amekwenda kinyume na hivo ambapo amesema:

“Sunnah ni kumswalia [maiti] iwe msikitini.”

na hakutaja kumswalia mahapa pa kuswalia. Haki ni vile tulivyotaja sisi katika Sunnah pamoja na kwamba inafaa kuliswalia ndani ya msikiti. Hayo ni kutokana na ile Hadiyth ya ´Aaishah. Kuchukulia kitendo hicho kwamba ilikuwa ni kwa jambo lilizuka kidharurah ni jambo liko mbali. Mambo yangelikuwa hivo basi lisingefichikana kwa bibi ´Aashah na wale mama wa waumini waliokuwa pamoja naye na hivyo wasingeliomba kuingizwa jeneza msikitini pasi na udhuru. Haya yako wazi – Allaah (Ta´ala) akitaka.

Ya tano: Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule mwenye kuliswalia jeneza msikitini basi hakuna juu yake kitu.”

as-Swahiyhah” (2352).

[1] al-Haafidhw amesema katika ”al-Fath”:

”Mahala pa kuswalia majeneza ilikuwa imeambatana na msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) upande wa mashariki.”

Maeneo mengine amesema (12/108):

”Mahala pa kuswalia ni sehemu ambayo alikuwa akiswalia ´iyd na majeneza. Ni upande wa al-Baqiy´ al-Gharqad.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 135-137
  • Imechapishwa: 07/10/2020