69- Inafaa kila jeneza moja kuliswalia swalah yake kivyake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilifanya hilo kwa wale mashahidi wa Uhud. Kumepokelewa Hadiyth mbili zifuatazo juu ya hilo:

Ya kwanza: ´Abdullaah bin az-Zubayr amesimulia, imekwishatangulia katika masuala ya 59, Hadiyh ya pili, ukurasa wa 72.

Ya pili: Ibn ´Abbaas amesimulia:

“Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposimama juu ya mwili wa Hamzah… aliamrisha juu yake akaandaliwa kuelekezwa Qiblah. Kisha akampigia Takbiyr tisa. Kisha akamkusanyia mashahidi wengine. Kila anapoletwa shahidi mwingine basi anamweka sambamba na Hamzah ambapo anamswalia yeye na wale mashahidi wengine pamoja naye mpaka anapomaliza kumswalia yeye na wale mashahidi wengine – aliswali swalah sabini na mbili.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “Mu´jam-ul-Kabiyr” yake (03/107, 108) kupitia kwa njia ya Muhammad bin Ishaaq ambaye alihadithiwa na Muhammad bin Ka´b al-Quradhwiy, al-Hakam bin ´Utaybah, kutoka kwa Miqsam na Mujaahid ambao wamesimulia kutoka kwake.

Cheni ya wapokezi hii ni nzuri. Wapokezi wote ni waaminifu. Muhammad bin Ishaaq ametaja kwa uwazi kwamba amehadithiwa. Kwa hiyo ikaondoka shubuha ya tadlisi yake. Inavyodhihirika ni kwamba Imaam as-Suhayliy na al-Haafidhw Ibn Hajar hawakuiona cheni ya wapokezi hii. al-Haafidhw amesema katika “at-Talkhiysw” (05/153, 154):

“Kuhusiana na maudhui haya ipo Hadiyth ya Ibn ´Abbaas ambayo ameipokea Ibn Ishaaq aliyesema: “Amenihadithia yule ambaye mimi simtuhumu, kutoka kwa Miqsam, ambaye ni mtumwa aliyeachwa huru na Ibn ´Abbaas, kutoka kwa Ibn ´Abbaas… “

Akaitaja Hadiyth mfano wake isipokuwa tu yeye amesema:

“[Takbiyr] saba” badala ya “[Takbiyr] tisa.”

Kisha akasema: “as-Suhayliy amesema:

“Ikiwa yule ambaye Ibn Ishaaq amemtaja kwa kutomuweka wazi ni al-Hasan bin ´Imaarah, basi huyo ni dhaifu. Vinginevyo hatambuliki na hivyo hayajengewi hoja.”

Kilichomfanya as-Suhayliy kusema hivo ni yale yaliyotokea katika utangulizi wa “Muslim”, kutoka kwa ash-Shu´bah kwamba al-Hasan bin ´Imaarah amemuhadithia, kutoka kwa al-Hakam, kutoka kwa Miqsam, kutoka kwa Ibn ´Abbaas aliyeeleza:

“Kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalia wauliwaji wa Uhud.” Mimi nikamuuliza al-Hakam ambapo akajibu: “Hakuwaswalia.”

Hata hivyo Hadiyth ya Ibn ´Abbaas imepokelewa kwa njia nyingine… “

Kisha nikazitaja baadhi yake na ndani yake hakukuwepo njia hii ya at-Twabaraaniy. Nayo inajulisha kuwa yule ambaye ametajwa kwa mafumbo katika upokezi ule si mtu ambaye kwamba hajulikani wala dhaifu. Bali ni mtu mwaminifu na anayetambulika. Naye si mwengine ni Muhammad bin Ka´b al-Quradhwiy au al-Hakam bin ´Utaybah au wote wawili kwa pamoja. Wala haya hayatotia dosari maneno ya al-Hakam katika upokezi wa Muslim:

“… wala hakuwaswalia.”

kwa sababu inawezekana al-Hakam alisahau kile alichosimulia kama ambavo jambo hilo limewatoke wengine mfano wake juu ya Hadiyth nyingi. Endapo tutakubali katika hali ya kwendana na mazungumzo kule kuikataa Hadiyth yake kunaitia dosari kusihi kutoka kwake, basi hatutokubali litatia dosari juu ya usahihi wa Hadiyth yenyewe midhali pia imepokelewa na mtu mwaminifu mwengine mbali na yeye. Haya yako wazi – Allaah (Ta´ala) akitaka.”

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” (05-225):

“Wamekubaliana kwamba bora ni kumpwekesha kila mmoja kwa swalah yake. Isipokuwa tu mtunzi wa “at-Tatimmah”. Yeye amekata kauli kwamba bora awaswalie wote mkupo mmoja kwa sababu kufanya hivo kuna kuyaharakisha mazishi, jambo ambalo limeamrishwa. Lakini madhehebu [ya Shaafi´iyyah] ni yale ya kwanza. Kwa sababu ndio yenye kutendewa kazi zaidi na ndio yenye kutarajiwa zaidi kukubaliwa inagwa kuna kuchelewesha sana. Allaah ndiye mjuzi zaidi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 133-135
  • Imechapishwa: 07/10/2020