67. Yeyote anayewataja Maswahabah kwa ubaya ni mzushi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Mwenye kumtukana mmoja katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamchukia kwa sababu ya kitu alichofanya au akayataja mabaya yake ni mtu wa Bid´ah mpaka awatakie rehema wote na asiwe na kinyongo na yeyote katika wao.

MAELEZO

Huu ni msingi mkuu katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, nao ni kubainisha msimamo wao kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunapaswa kufuata mfumo huu. Kila muislamu wa kiume na wa kike analazimika kufuata mfumo huu. Haifai kwa yeyote kutaja mabaya yao. Hata kama wanaweza kuteleza basi mapungufu yao hayana maana yoyote ukiyalinganisha na matendo yao mazuri. Haijuzu kwa yeyote kuingilia kati vile vita vilivyotokea baina yao, magomvi na mfano wa hayo. Haijuzu kabisa kumtia mapungufu Swahabah yeyote wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa hali yoyote ile. Kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza hayo na akasema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake lau mmoja wenu atajitolea dhahabu mfano wa mlima wa Uhud basi hatofikia viganja viwili vya mikono vilivyojazwa na mmoja wao wala nusu yake.”[1]

Utaona jinsi Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanawaombea radhi Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanaona kuwa kuwapenda ni faradhi ambayo amefaradhisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wamewaridhia kwa nje na kwa ndani na wanakomeka na mapungufu yao. Wanatambua kuwa yale yote yanayosemwa kuhusu Maswahabah kuna ambayo ni ya uwongo mtupu na hivyo hayatakiwi kusadikishwa, mengine yameongezwa chumvi au masimulizi yaliyopunguzwa ambayo hayatakiwi kuchukuliwa kazi. Yale yaliyosihi kuwa wameyafanya, wanawajengea dhana njema na hawaingii katika mada hiyo. Makosa yao ni yenye kufunikwa na yale mazuri yao mengi. Maswahabah wana sifa nyingi za kipekee na maalum, ikiwa ni pamoja na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wenu ni karne yangu, kisha wale watakaofuata, kisha wale watakaofuata.”[2]

Kwa ajili hiyo hakuna yeyote yule ambaye anawatia mapungufu Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa tu mzushi mpotofu ambaye amepinda kutokana na mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] al-Bukhaariy (3673) na Muslim (2540).

[2] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 150-151
  • Imechapishwa: 23/06/2026