Imaam Ahmad amepokea katika “al-Musnad” yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anashangazwa na kijana asiyevutikiwa na mambo ya upuuzi.”

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu saba Allaah atawaweka kwenye kivuli cha ´Arshi ya Allaah siku ambayo hakutokuwa kivuli isipokuwa kivuli Chake; kiongozi mwadilifu, kijana aliyekulia katika kumtii Allaah, mtu ambaye moyo wake umefungamana na misikiti, watu wawili waliopendana kwa ajili ya Allaah wakakutana kwa ajili ya Allaah na kuachana kwa ajili ya Allaah, mtu aliyeitwa na mwanamke aliye na nafasi na mrembo lakini akasema: “Mimi namwogopa Allaah, Mola wa walimwengu”, mtu aliyetoa swadaqah akaificha mpaka mkono wake wa kushoto usijue kilichotolewa na mkono wake wa kulia na mtu mwenye kumkumbuka Allaah akiwa faragha na akatokwa na machozi.”

Watu aina saba hawa wanastahiki kufunikwa na kivuli cha Allaah kutokana na subira yao kamilifu na uzito wao.

Mfalme anasubiri kwa uadilifu pamoja na kuwa ana uwezo wa kudhulumu na kuwalipiza raia wake kisasi.

Kijana anasubiri katika kumtii Allaah na kwenda kinyume na matamanio yake.

Mwanaume anasubiri kulazimiana na msikiti.

Mtoa swadaqah anasubiri kuificha swadaqah yake pamoja na kuwa anaweza kuionyesha.

Mwitwaji anasubiri juu ya machafu pamoja na urembo wa mwanamke.

Watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah wanasubiri wanapoungana na wanapotengana.

Mwenye kulia kwa ajili ya kumwogopa Allaah anasubiri na kutowaonyesha wengine kulia kwake.

Mambo yote haya ni magumu. Kuwa na ustahamilivu kwa mambo haya ni kwa msaada wa mafanikio ya Allaah, fadhila na wema Wake na ni subira iliyokuwa njema.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 149
  • Imechapishwa: 05/11/2016