Katika kumuamini Allaah kunaingia vilevile kuamini yale yote aliyoyawajibisha na kuyafaradhisha kwa waja Wake katika nguzo za Uislamu tano za dhahiri; nazo ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba ya Allaah tukufu kwa mwenye kuweza kuiendea na mambo mengine ambayo yameletwa na Shari´ah Takasifu.

Nguzo muhimu na kubwa zaidi ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah kunapelekea kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee na kumkanushia nayo asiyekuwa Yeye. Hii ndio maana ya “Laa ilaaha illa Allaah”. Maana yake ni hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Kila kinachoabudiwa badala ya Allaah katika watu, Malaika, jini na vyenginevyo ni vyenye kuabudiwa kwa batili. Muabudiwa wa haki ni Allaah peke yake. Amesema (Subhaanah):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili.” (22:62)

Tumetangulia kusema kuwa Allaah (Subhaanah) amewaumba majini na watu kwa ajili ya msingi wa misingi huu na akawaamrisha nao. Kadhalika amewatuma Mitume na akateremsha vitabu kwa lengo hilo. Hivyo basi zingatia hilo vizuri ili ipate kukubainikia ule ujinga mkubwa waliyotumbukia kwao waislamu juu ya msingi wa misingi huu na matokeo yake wakamuabudu Allaah pamoja na wengine na vilevile wakawatekelezea wengine haki ambayo ni maalum Kwake. Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 05
  • Imechapishwa: 30/05/2023