67. Kuunganisha swalah papo hapo kwa anayekusanya

Swali 67: Ni ipi hukumu ya kuunganisha papo hapo (الموالاة) kati ya swalah mbili ikiwa watachelewesha kwa kitambo kinachozingatiwa ni upambanuzi kati ya swalah mbili  kisha baadaye wakakusanya?

Jibu: Kilicho cha wajibu wakati mtu anapokusanya katika ule wakati wa swalah ya kwanza (جمع التقديم) ni kuunganisha papo hapo kati ya swalah mbili. Hapana vibaya kupambanua kitambo kidogo kwa mujibu wa desturi kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya hilo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Maoni ya sawa ni kwamba manuizi sio sharti, kama ilivyotangulia katika jibu la swali lililotangulia la 66. Kuhusu kukusanya katika ule wakati wa swalah ya pili (جمع التأخير) wigo wake ni mpana. Kwa sababu swalah ya pili inaswaliwa ndani ya wakati wake. Lakini bora ni kuunganisha papo hapo kati ya swalah hizo mbili kwa ajili ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jambo hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 71
  • Imechapishwa: 13/09/2022