Adhabu au neema za kaburi ni haki kwa udhahiri wa Qur-aan, Sunnah iliyosema hilo wazi na maafikiano ya Ahl-us-Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Suurah “al-Waaqi´ah”:

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ

“Basi mbona roho ifikapo kooni nanyi kipindi hicho mnatazama.”[1]

 Mpaka alipofikia kusema:

فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ 

“Basi akiwa miongoni mwa waliokurubishwa. Basi mapumziko ya raha na manukato na Pepo yenye neema.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuomba Allaah kinga kutokamana na adhabu ya kaburi na akauamrisha Ummah wake kufanya hivo[3]. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth ya al-Baraa´ bin ´Aazib iliyotangaa kuhusu kisa cha fitina ya kaburi ambapo alisema kuhusu waumini:

“Atanadi mwenye kunadi kutoka juu mbinguni akisema: “Amesema kweli mja wangu. Mtandikieni godoro kutoka Peponi, mfungulieni mlango wa Peponi, hukunjuliwa ndani ya kaburi lake kiasi cha upeo wa macho yake mpaka akaona nyumba yake Peponi na akafikiwa na upepo na harufu yake.”

Kuhusu ambaye ni kafiri:

“Atanadi mwenye kunadi kutoka juu mbinguni akisema: “Amesema kweli mja wangu. Mtandikieni godoro kutoka Motoni, mfungulieni mlango wa Motoni ambapo atajiliwa na joto na sumu yake na kaburi lake litafanywa kumbana mpaka zikutane mbavu zake.”[4]

Hadiyth hiyo ameipokea Ahmad na Abu Daawuud.

Salaf na Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu ya kuthibitisha adhabu na neema za kaburi. Hayo yametajwa na Ibn-ul-Qayyim katika “Kitaab-ur-Ruuh”.

[1] 56:83-84

[2] 56:88-89

[3] Muslim (590, 134, 903, 08) al-Bukhaariy (1049).

[4] Ameipokea Ahmad (04/287, 288, 295, 296) na Abu Daawuud (4753).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 28/11/2022