Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Adhabu ya kaburi na neema zake ni haki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba kinga kutokamana nayo na akaamrisha hilo katika kila swalah. Fitina ya kaburi ni haki, maswali ya Munkar na Nakiyr ni haki na kufufuliwa baada ya kufa ni haki – na hilo ni baada ya Israafiyl (´alayhisSalaam) kupuliza parapanda:

فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ

”Basi tahamaki wanatoka makaburini mwao wakienda mbiombio kwa Mola wao.”[1]

MAELEZO

Fitina maana yake kilugha ni mtihani. Fitina ya kaburi ni maiti kuulizwa kuhusu Mola, dini na Mtume Wake. Ni jambo limethibiti kwa Qur-aan na kwa Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu akihojiwa ndani ya kaburi basi atashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Hiyo ndio maneno Yake (Ta´ala):

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah.”[3]

Waulizaji ni Malaika wawili. Hilo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mja anapowekwa ndani ya kaburi lake na watu wake wakamuacha husikia mlio wa viatu vyao. Atajiliwa na Malaika wawili ambao watamkaza chini.”[4]

Ameipokea Muslim.

Majina yao ni Munkar na Nakiyr. Hayo yamepokelewa na at-Tirmidhiy kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). at-Tirmidhiy amesema:

“Nzuri na geni.”

al-Albaaniy amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni nzuri na ni kwa mujibu wa sharti za Muslim.”[5]

Wataohojiwa ni wale waumini na makafiri waliokwishabaleghe kutoka katika Ummah huu na nyumati zingine. Kuna maoni tofauti kuhusu kuhojiwa kwa wale ambao hawajabaleghe. Udhahiri wa maneno ya Ibn-ul-Qayyim katika kitabu “ar-Ruuh” ni kwamba maoni yenye nguvu ni kuwa watahojiwa. Anabaguliwa katika hali hiyo ambaye amekufa shahidi kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na an-Nasaa´iy[6]. Vilevile anabaguliwa yule ambaye amekufa hali ya kulinda mipaka ya waislamu kutokana na Hadiyth aliyoipokea Muslim[7].

[1] 36:51

[2] 14:27

[3] al-Bukhaariy (1369) na Muslim (3871, 73).

[4] al-Bukhaariy (1338) na Muslim (2870, 70).

[5] at-Tirmidhiy (1071), Ibn Hibbaan (780) – Mawaarid, Ibn Abiy ´Aaswim katika “as-Sunnah” (864). at-Tirmidhiy amesema:

”Nzuri na geni.”

al-Albaaniy ameisema kuwa ni nzuri katika ”Dhwilaal-ul-Jannah fiy Takhriyj-is-Sunnah” (864) na amesema katika ”as-Swahiyhah” (1391):

”Cheni ya wapokezi wake ni nzuri na wanamme wake wote ni waaminifu na ni wapokezi wa Muslim.”

[6] Ameipokea an-Nasaa´iy (01/279). 

[7] Muslim (1913, 163).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 111-112
  • Imechapishwa: 28/11/2022