65. Radd juu ya shubuha wanayotumia Mu´tazilah na vifaranga vyao kupinga kuonekana kwa Allaah Aakhirah

Kuhusu Mu´tazilah na waliofuata mkondo wao wanapinga kuonekana kwa Allaah, kama ilivyo kawaida yao. Kwa sababu hawazisadikishi Hadiyth na wanafuata akili na fikira zao na wanatumia zile dalili zisizokuwa wazi kutoka ndani ya Qur-aan. Kwa mfano maneno Yake (Ta´ala) kuhusu Muusa:

قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَن تَرَانِي

“Akasema: “Mola wangu! Nionyeshe ili nikutazame.” Akasema: “Hutoniona! Lakini tazama jibali, ukitulia mahala pake, basi utaniona.”[1]

Wamesema kuwa maneno:

 لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!”

yanakanusha kuonekana. Kwa hiyo ni dalili yenye kuonyesha kuwa Allaah haonekani. Tunaraddi hilo kwa njia mbili:

1- Ingelikuwa kuonekana kwa Allaah ni jambo lisilojuzu basi Muusa asingeliomba. Kwa sababu Muusa ni Mtume na msemezwa wa Allaah na haiwezekani akaomba kitu kisichojuzu. Ni dalili inayoonyesha kwamba kuonekana kwa Allaah ni jambo linalofaa. Lakini hatoonekana hapa duniani. Kwa sababu viumbe hawana nguvu za kumuona katika dunia hii. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah akampigia mfano:

قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا

”Akasema: “Mola wangu! Nionyeshe ili nikutazame.” Akasema: “Hutoniona! Lakini tazama jabali, likitulia mahali pake, basi utaniona.” Basi Mola wako alipojidhihirisha katika jabali, alilijaalia kuwa lenye kupasukapasuka.”[2]

Bi maana akakosa fahamu. Ni dalili inayofahamisha kuwa Muusa hana uwezo wa kumuona Allaah katika dunia hii. Kila kiumbe hakiwezi kumuona Allaah katika dunia hii kwa sababu ya udhaifu wa viumbe katika dunia hii. Ama Peponi Allaah atawapa nguvu waumini za kumuona Mola Wao (Subhaanahu wa Ta´ala).

2- Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakumwambia Muusa:

إني لا أرى

“Mimi sionekani.”

Bali alisema:

لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!”

Bi maana katika dunia hii. “Lani” haipelekei katika ukanushaji wa moja kwa moja. Lan inapelekea katika ukanushaji wa kipindi fulani. Kwa ajili hiyo Ibn Maalik amesema katika “al-Kaafiyah ash-Shaafiyah”[3]:

Mwenye kuona kwamba ukanushaji wa “lan” ni wa milele

maneno yake yarudishe na uunge mkono mengine

Kwa hiyo makanusho ya “Lan” sio ya milele. Kwa ajili hiyo Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kuhusu mayahudi:

وَلَن يَتَمَنَّوْهُ أَبَدًا

“Hawatoyatamani kamwe.”[4]

Bi maana kifo. Lakini Aakhirah watatamani kufa. Amesema (Ta´ala):

وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ ۖ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ

“Wataita: “Ee Maalik! Atumalize tufe Mola wako.” Atasema: “Hakika nyinyi ni wenye kubakia kuishi humo.”[5]

Siku ya Qiyaamah watatamani kufa ingawa hapa duniani hawakuyatamani. Kwa hiyo ni dalili inayoonyesha kuwa “Lan” ni makanusho yaliyoachiwa ambayo hayapelekei umilele. Ni ukanushaji wa muda maalum. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

لَن تَرَانِي

“(Lan) hutoniona!”

Bi maana duniani. Kwa hiyo hawana mashiko yoyote katika Aayah hii.

[1] 07:143

[2] 07:143

[3] Tazama ”Sharh al-Kaafiyah ash-Shaafiyah” (02/205).

[4] 02:95

[5] 43:77

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 17/05/2021