65. Kufufuliwa kwa watu baada ya kufa na dalili ya hilo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya watu kufa, watafufuliwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”[1]

وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا

”Na Allaah amekuotesheni kutoka katika ardhi mimea; kisha atakurudisheni humo [ardhini] na atakutoeni [tena upya] mtoke.”[2]

Baada ya kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa matendo yao. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.”[3]

Yule mwenye kukanusha kufufuliwa anakufuru. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.”[4]

Allaah ametuma Mitume wote wakiwa ni wenye kutoa bishara njema na kuonya. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

“Mitume wenye kutoa bishara njema na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa ya Mitume. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[5]

MAELEZO

Maneno Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”

Bi maana ardhini. Hii ni dalili ya kufufuliwa na baada ya kufufuliwa watafanyiwa hesabu na kulipwa kutokana na matendo yao; yakiwa ni mazuri watalipwa mazuri, na yakiwa mabaya watalipwa mabaya. Amesema (Ta´ala):

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri uzito wa chembe ataiona.”[6]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule mwenye kukanusha kufufuliwa anakufuru.”

Mwenye kusema kama wanavosema wanafalsafa kwamba roho ndio zitafufuliwa ni kafiri. Roho zitabakia. Roho ya muumini baada ya kufa inapelekwa Peponi na inakuwa na uhusiano na mwili. Roho ya kafiri baada ya kufa inapelekwa Motoni na inakuwa na uhusiano na mwili. Viwiliwili huoza. Roho hubaki ima katika neema au adhabu. Ni lazima kuamini kufufuliwa kwa viwiliwili. Ambaye haamini jambo hilo ni kafiri.

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.”

Mfano mwingine ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَأْتِينَا السَّاعَةُ ۖ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ عَالِمِ الْغَيْبِ

”Na wale waliokufuru wakasema: ”Saa haitotufikia.” Sema: ”Bila shaka! Naapa kwa Mola wangu itakufikieni, mjuzi wa mambo yaliyofichikana.””[7]

وَيَسْتَنبِئُونَكَ أَحَقٌّ هُوَ ۖ قُلْ إِي وَرَبِّي إِنَّهُ لَحَقٌّ

”Wanakuuliza: ”Je, hayo ni kweli?” Sema: ”Ndio, naapa kwa Mola wangu! Hakika hayo bila shaka ni kweli.””[8]

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

”Allaah ametuma Mitume wote wakiwa ni wenye kutoa bishara njema na kuonya.”

Allaah amewatuma Mitume wote hali ya kuwa ni wenye kutoa bishara njema na wenye kuonya. Hili ndio jukumu la Mitume; wanawapa bishara njema ambao wanawatii na wanaomwabudu Allaah pekee kwamba wataingia Peponi, na wanawaonya wale wenye kuwaasi kutokana na Moto. Mtunzi wa kitabu amelifunga kila suala kwa dalili yake. Ametaja dalili ya hilo ambayo ni maneno Yake (Ta´ala):

كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ

“Watu walikuwa ummah mmoja kisha Allaah akawatuma Mitume hali ya kuwa ni wabashiriaji na waonyaji na Akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki ili kihukumu kati ya watu katika ambayo wamekhitilafiana kwayo.”[9]

[1] 20:55

[2] 71:17-18

[3] 53:31

[4] 64:07

[5] 04:165

[6] 99:07-08

[7] 34:03

[8] 10:53

[9] 02:213

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 19/02/2023