61- Ni lazima kuswali kwa mkusanyiko katika swalah ya jeneza kama ilivyo lazima katika swalah nyenginezo za faradhi. Hilo ni kutokana na dalili mbili:

Ya kwanza: Kudumu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo.

La pili: Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Hayo tuliyoyaja hayachafuliwi na swalah ya Maswahabah kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu mmojammoja na hakuna yeyote ambaye aliwaongoza. Kwa sababu hii ni qadhiya maalum ambayo mtazamo wake hautambulikani. Haijuzu kwa ajili yake tukaacha yale ambayo alidumu nayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika uhai wake wote uliyobarikiwa khaswa ukiongezea kwamba qadhiya iliyotajwa haikupokelewa katika cheni ya wapokezi ambayo ni Swahiyh ambayo mtu kwayo anaweza kujengea hoja ingawa imepokelewa kupitia njia zinazotiana nguvu[1]. Tukiweza kuyaoanisha kati yake na yale tuliyotaja katika uongofu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kukusanyika kwa ajili ya jeneza basi itakuwa ni vyema. Vinginevyo uongofu wake ndio wenye kuthibiti na wenye kuongoka zaidi.

Likiswaliwa jeneza na mtu mmojammoja basi faradhi itadondoka na watapata dhambi kwa kule kuacha kwao swalah ya mkusanyiko – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´” (05/314):

“Inafaa kuliswalia jeneza mtu mmojammoja bila kuwepo kwa tofauti. Sunnah ni kuliswalia kwa mkusanyiko. Hilo ni kutokana na Hadiyth zinazotambulika katika as-Swahiyh juu ya jambo hilo pamoja na maafikiano ya waislamu.”

62- Idadi ya chini kabisa iliyopokelewa katika kufungika kwa mkusanyiko ni watu watatu. Imekuja katika Hadiyth ya ´Abdullaah bin Abiy Twalhah:

“Abu Twalhah alimwita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda kwa ´Umayr bin Abiy Twalhah wakati alipokufa ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjia na akamswalia nyumbani kwao. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatangulia mbele, Abu Twalhah alikuwa nyuma yake, Umm Sulaym alikuwa nyuma ya Abu Twalhah na hapakuwa mwengine zaidi yao.”

Ameitoa al-Haakim (01/365) na al-Bayhaqiy (04/30,31) amepokea kutoka kwake. al-Haakim amesema:

“Hii ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim na ni Sunnah geni juu ya kuhalalisha wanawake kuyaswalia mejeneza.” adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

Iko kwa mujibu wa sharti za Muslim peke yake kwa sababu ndani yumo ´Imaarah bin Ghuzayyah. al-Bukhaariy hakumtolea chochote isipokuwa katika hali ya kuiwekea taaliki. al-Haythamiy amesema juu yake katika “al-Majma´” (03/34):

“Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Kabiyr” na wapokezi wake ni wapokezi Swahiyh.”

Ina shahidi kutoka katika Hadiyth ya Anas kwa maana yake.

Ameipokea Imaam Ahmad (02/217).

[1] Ameitoa al-Bayhaqiy katika ”Sunan” yake (04/30) kutoka humo Hadiyth mbili. Moja katika hizo iko kwa Ibn Maajah (01/498, 500). Ahmad (01/81) amepokea Hadiyth ya tatu na al-Haafidhw akainyamazia katika “at-Talkhiysw” (05/187). Wapokezi wake ni waaminifu na ni wapokezi wa Muslim isipokuwa tu Abu ´Usaym. al-Baghawiy amesema:

“Sijui kama ni Swahiyh au hapana.”

Kuhusiana na maudhui haya zipo Hadiyth nyenginezo. Amezitoa al-Haafidhw katika kitabu kilichotajwa kisha akasema:

“Ibn Dihyah amesema: “Sahihi ni kwamba waislamu walimswalia mmojammoja na hakuna yeyote aliyewaongoza. ash-Shaafi´iy ametaka kauli kwa hilo pia. Akasema: “Hilo ni kutokana na utukufu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – namtoa fidia kwake baba na mama yangu – na jengine ni kwa sababu ya kushindana kwao asibebe jukumu la uimamu yeyote katika kumswalia. Allaah ndiye mjuzi zaidi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 124-127
  • Imechapishwa: 13/08/2020