Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:
Siri ya masuala ni kwamba akisema: “Mimi simshirikishi Allaah na chochote”. Mwambie: “Nieleze, ni nini kumshirikisha Allaah? Nifasirie.” Akisema: “Ni kuabudu masanamu” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kuabudu masanamu?” Akisema: “Mimi siabudu isipokuwa Allaah pekee” Mwambie: “Nieleze, ni nini maana ya kumuabudu Allaah pekee? Nifasirie.” Akikueleza [kubainishia] kama ilivyoeleza Qur-aan, ndio kinachotakikana. Na ikiwa hajui, vipi atadai kitu na yeye hakijui?
Na akikubainishia kinyume na maana yake, mbainishie Aayah zilizo za wazi za maana ya kumshirikisha Allaah na ´ibaadah ya kuabudu masanamu na kwamba ndio yaleyale wayafanyayo hii leo. Mbainishie pia kuwa ´ibaadah anayotekelezewa Allaah pekee ndio yale wanayotupinga kwayo na kutupigia kelele. Wanatupigia mayowe kama walivyopiga mayowe ndugu zao pale waliposema:
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا
“Amewafanya miungu wote hawa kuwa mungu Mmoja?” (38:05)
MAELEZO
Akisema kuwa yeye hamshirikisha Allaah na chochote, muulize ni nini maana ya shirki. Akisema kuwa ni kuyaabudia masanamu, muulize ni nini maana ya kuabudu masanamu. Endelea kujadiliana naye kwa ile njia tuliyoitanguliza.
Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:
“Ni kuabudu masanamu… “
Mshirikina huyu akidai kuwa yeye hamuabudu isipokuwa Allaah pekee, muulzie ni nini maana ya kumuabudu Allaah pekee. Hapo hatotoka nje ya hali tatu:
1 – Kufasiri hilo kwa mujibu wa Qur-aan. Hili ndilo linalotakikana na lenye kukubaliwa. Hali kadhalika itabaini kuwa hakumuabudu Allaah pekee, kwa sababu amemshirikisha.
2 – Hajui maana yake. Katika hali hii ataulizwa ni vipi utaweza kudai jambo na wewe hujui maana yake. Ni vipi ataweza kujihukumu kwa jambo ilihali hukumu juu ya jambo ni tawi la ile sura yake?
3 – Afasiri kumuabudu Allaah kwa njia ya kimakosa. Hapa kosa lake linatakiwa kubainishwa. Mtu abainishe uelewa wa Kishari´ah wa maana ya shirki na kwamba ndio yaleyale wanayofanya ilihali wao wanasema kuwa wanamuabudu Allaah pekee.
Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):
“Ni nini maana ya kuabudu masanamu?”
Vivyo hivyo abainishiwe kuwa wanatukemea kwa sababu tunamuabudu Allaah pekee. Wanatukaripia kwa jambo hilo kama walivyofanya mababu zao pindi walipomwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ وَانطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ يُرَادُ مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ
“Amewafanya miungu wote hawa kuwa mungu Mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno! Na wakaondoka wakuu miongoni mwao [wakisema]: “Nendeni na subirini juu ya miungu yenu, hakika hili ni jambo linalotakwa. Hatukusikia haya katika dini ya mwisho, haya si chochote isipokuwa ni jambo lilozushwa tu.”” (38:05-07)
- Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 73-75
- Imechapishwa: 25/11/2023
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)