64. Shirki ya watu wa kale ni khafifu kuliko ya watu wa leo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mlango wa kumi na moja

Shirki ya watu wa kale ni khafifu kuliko ya watu wa leo

Ukishajua waliitalo washirikina katika zama zetu hizi “itikadi” ndio shirki iliyotajwa katika Qur-aan na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapigana na watu kwa ajili yake, basi ujue kuwa shirki ya watu wa mwanzo ni khafifu kuliko shirki ya watu wa zama zetu kwa mambo mawili.

1 – Watu wa mwanzo walikuwa hawashirikishi na wala hawawaombi Malaika, mawalii na masanamu pamoja na Allaah isipokuwa wakati wa raha. Ama wakati wa shida, walikuwa ni wenye kumtakasia Allaah maombi. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Na inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Anapokuokoeni katika nchikavu, mnakengeuka. Na mtu daima ni mwingi wa kukanusha.” (17:67)

MAELEZO

Ukishatambua maana ya ´ibaadah na kwamba yale waliyomo washirikina wa sasa ndio hali ileile waliokuwemo washirikina wa zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi utaona kuwa shirki ya watu wa sasa ni mbaya zaidi kuliko wale ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita. Hili linabainika kwa mambo mawili:

1 – Washirikina wa leo wanamshirikisha Allaah ni mamoja wakati wa shida na wakati wa raha. Ama wale washirikina ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitumwa kwao, walikuwa wakishirikisha tu wakati wa raha na wakimtakasia ´ibaadah Allaah wakati wa shida. Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Na inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa Yeye pekee. Anapokuokoeni katika nchikavu mnakengeuka. Na mwanaadamu daima ni mwingi wa kukanusha.”

Wanapopanda jahazi, wanamuomba Allaah na si mwengine. Lakini wanapofika nchikavu, ndipo wanamshirikisha. Hili ni mosi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 76
  • Imechapishwa: 25/11/2023