63. Faida tatu za kuamini mipango na makadirio

5 – Kuhusu faida ya kuamini mipango na makadirio. Kuamini mipango na makadirio kuna faida nyingi:

1 – Faida kubwa kuliko zote ni kukamilisha nguzo za imani. Anayepinga mipango na makadirio hakukamilisha nguzo za imani ambazo amefasiri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mtu kuziamini:

“Kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na kuamini makadirio ya kheri na ya shari yake.”

2 – Mja anakuwa si mwenye kutilia manani mawazo na khofu. Anakuwa ni mwenye kwenda zake na huku akitambua kuwa kile alichomkadiria Allaah kitakuja tu, ni mamoja akae chini au asikae. Kwa ajili hii pindi wanafiki siku ya Uhud waliposema:

الَّذِينَ قَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُوا لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا ۗ قُلْ فَادْرَءُوا عَنْ أَنفُسِكُمُ الْمَوْتَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Wale waliowaambia ndugu zao nao wakakaa [hawakwenda vitani]: “Lau wangelitutii basi wasingeliuawa.” Sema: “Basi ziondoleeni nafsi zenu mauti mkiwa ni wakweli.” (03:168)

Kukaa nyumbani hakumzuii mtu kutokana na kufa kama ambavyo vilevile kutoka kwenda katika Jihaad hakumfanyi mtu akafa au kuleta kifo ikiwa Allaah hakukikadiria. Ni kweli kwamba ni sababu, lakini ikiwa Allaah hakukikadiria hakina athari na wala hakileti natija yoyote. Ni wangapi wametoka kwenda vitani na wamerudi wakiwa salama salimina. Khaalid bin Waliyd (Radhiya Allaahu ´anh) yalipomfika mauti alisema:

“Mwilini mwangu hakuna sehemu kiasi cha shibri moja isipokuwa kuna kovu la kipigo.”[1]

Alikuwa ni mtu anatamani sana kufa shahidi. Alishuhudia vita vikubwa na akatamani sana auawe katika njia ya Allaah. Lakini hata hivyo Allaah hakumwandikia hivo.

Kuamini mipango na makadirio kunamfanya mtu kuwa na ushujaa, kutangulia na kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kukaa hakumfidishi mtu kitu. Amesema (Ta´ala):

قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ

“Sema: “Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuwawa kwenye mahali pa kuangukia wafe.” (03:15)

أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِككُّمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِي بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ

“Popote mtakapokuwa yatakufikieni mauti, japo mkiwa katika ngome zilizo na nguvu.” (04:78)

Mipango ni lazima itekelezeke na itokee.

Kwa hivyo hakuna faida yoyote ya mtu kukaa na kuacha kufanya sababu za faida na kuziepuka sababu mbaya. Haya yanamfanya mtu kuwa na ujasiri na ushujaa wa kumuamini Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile kunamfanya mtu asiwe na mashaka, wasiwasi na kuamini mikosi inayowapata watu wengi. Kunamwondoshea mtu kuwa na wasiwasi. Kwa ajili watu wa imani hawakuwa wakichelewa katika kutafuta mambo yaliyo na kheri na faida. Kwa sababu walikuwa ni wenye kuamini mipango na makadirio. Hawakuwa ni wenye kuogopa kufa na kuuawa. Ikiwa kifo kimeshaandikwa kwako kitakujia tu, hata kama hutokiendea, na kama hujaandikiwa hakitokufika hata kama utakuwa katika khatari ilio kubwa.

3 – Mtu havunjiki moyo na kukata tamaa pindi anapofikwa na tatizo. Kwa sababu anaamini kuwa kimetokea kwa mipango na makadirio ya Allaah. Hili linasahilisha kukabiliana na matatizo. Hivyo mtu anakuwa si mwenye kukata tamaa hajipigi kwenye mashavu, hapasui nguo na haiti kwa wito wa kipindi kabla ya kuja Uislamu. Kinyume chake anakuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema; na hao ndio wenye kuongoka.” (02:155-157)

Ni wale ambao wanapofikwa na matatizo hawazilaumu nafsi zao na kusema ni kwa sababu hii na ile. Wanaridhia mipango na makadirio ya Allaah na kwamba tatizo hilo lilikuwa lenye kutokea kwa hali yoyote ile aliyokuwa Allaah kishakadiria. Kilichokadiriwa kinatokea kwa idhini ya Allaah. Wanasema:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Endapo utafikwa na jambo usisemi “lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa na kadhaa”. Badala yake unatakiwa kusema “Allaah ameshakadiria. Anafanya alitakalo.””[2]

Haya yanamsahilishia mtu matatizo yake na badala yake anaridhia na kujisalimisha na mipango na makadirio ya Allaah. Hizi ni faida tatu zinazopatikana kwa kuamini mipango na makadirio:

1 – Kukamilisha nguzo za imani.

2 – Kuamini mipango na makadirio kunamfanya mtu kuwa na nguvu, ushujaa na kuwa msitari wa mbele katika kufanya mambo ya kheri.

3 – Kuamini mipango na makadirio kunamuwepesishia muislamu yale matatizo yanayomfika.

Kuhusiana na ambaye haamini mipango na makadirio utamuona ni mwenye kuvunjika moyo na kukata tamaa, kukasirika na hufikwa na yakumfika.

[1] Taariykh Dimashq (16/273) ya Ibn ´Asaakir

[2] Muslim (34) na (2667)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 148-151
  • Imechapishwa: 12/01/2024