62. Kuamini mipango na makadirio hakupingani na kufanya sababu

Kuamini mipango na makadirio na kufanya sababu ni mambo mawili yasiyopingana. Wewe unachotakiwa ni kuamini anayotaka Allaah huwa na asiyotaka hayawi. Lakini hata hivyo usiache kufanya sababu. Bali unatakiwa kutafuta riziki, kuoa, kufanya biashara na kuhangaika na kutafuta riziki. Usisemi kuwa wewe unategemea mipango na makadirio na kwamba ikiwa kitu kimeshakadiriwa kwako, basi kitakujia, na kama hukukadiriwa nacho, hakitokujia. Haya hayasemwi na mtu mwenye akili. Hata wanyama – kwa maumbile yao – wanatoka na kwenda kutafuta riziki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi ´alayhi wa sallam):

“Lau kweli mngelikuwa mnamtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea, basi angalikuruzukuni kama anavyomruzuku ndege: anatoka asubuhi akiwa hana kitu na anarudi jioni tumbo limejaa.”[1]

Ndege habaki ndani ya chicha lake. Anaruka na kwenda kutafuta riziki.

Kwa hivyo hakuna mgongano kati ya kuamini mipango na makadirio na kufanya sababu. Wenye kuamini hivi ni Jabriyyah.

Lakini pamoja na haya yote sababu haipwekeki katika kuleta natija. Msababishi ni Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hii ni Radd kwa Qadariyyah. Hatupindukii mjpaka katika kuthibitisha sababu, kama walivyofanya Qadariyyah, na wala hatupindukii mipaka katika kuikanusha, kama walivyofanya Jabriyyah. Kufanya sababu ni jambo linalotakikana. Amesema (Ta´ala):

فَابْتَغُوا عِندَ اللَّـهِ الرِّزْقَ

“Basi tafuteni riziki kwa Allaah.” (29:17)

وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ

“Tafuteni kutoka katika fadhilah za Allaah.” (62:10)

Allaah ameamrisha swalah, swawm na kufanya mema mbalimbali. Haya ni katika kufanya sababu. Vivyo hivyo amekataza sababu za shari kama kufuru, maasi na machafu.

Kuamini mipango na makadirio haina maana kwamba sasa unatakiwa kuacha kufanya sababu. Unatakiwa kuendelea kutafuta na wakati huohuo kuamini ya kwamba ikiwa Allaah amekuandikia jambo, basi litakujia. Hutojiwa na jambo ilihali umekaa tu. Ni lazima ufanye sababu. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pupia lile lenye kukufaa na umtake msaada Allaah na wala usikate tamaa. Endapo utafikwa na jambo usisemi “lau ningefanya kadhaa ingelikuwa kadhaa na kadhaa”. Badala yake unatakiwa kusema “Allaah ameshakadiria. Anafanya alitakalo.””[2]

Wewe unachotakiwa ni kufanya sababu. Ukifikia natija himdi zote zinamrudilia Allaah, na usipofikia natija mshukuru Allaah na ujisalimishe ya kwamba Allaah alikuwa hakukuandikia jambo hilo. Hadiyth hii iko wazi katika kufanya sababu na kwamba kuamini mipango na makadirio haina maana mtu aache kufanya sababu au kwamba kufanya sababu kunatosheleza katika kuleta natija ya mambo, kama wanavyosema Mu´tazilah. Mja hufanya sababu – mema au maasi – na natija inakuwa mikononi mwa Allaah. Yeye ndiye ambaye huzalisha natija na msababishaji wa sababu zinazofanywa.

[1] at-Tirmidhiy (2344), Ibn Maajah (4164), Ahmad (01/30) na wengineo. Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy

[2] Muslim (34) na (2667)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 146-148
  • Imechapishwa: 12/01/2024