62. Ulazima wa kuwa na subira mpaka wakati wa kufa

Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba maadamu muislamu mwenye kubaleghe na ambaye matendo ni yenye kumuwajibikia bado anaishi katika dunia hii na kalamu inaandika juu yake, ni lazima awe na subira katika hali zote zile.

Kama ameamrishwa basi ni lazima atekeleze maamrisho na kusubiri. Kama amekatazwa ni lazima ayaepuke makatazo na kusubiri. Anapofikwa na msiba ni lazima kuwa na subira. Anapopata neema ni lazima kumshukuru Aliyemneemesha nayo na kusubiri. Ikiwa mtu hana namna ya kuziepuka hali hizi, basi ni lazima asubiri mpaka pale atapokufa.

Mtu akiuliza kama mtu anahitajia kuwa na subira juu ya neema, atajibiwa ndio. Neema ni katika mtihani. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَمَّا الْإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ

“Ama mwanadamu pale Mola wake anapomtia mtihanini, akamkirimu na kumneemesha, husema: “Mola wangu amenikirimu.” 89:15

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ

”Bila ya shaka Tutakujaribuni mpaka tutambue wenye wale wenye kupambana na kufanya bidii miongoni mwenu na wenye kuvuta subira na Tutazijaribu habari zenu [kuona ukweli wake zilivyo].” 47:31

وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ كَلَّا

“Ama Anapomtia mtihanini, akamdhikishia riziki yake, husema: “Mola wangu ameniabisha. Sivyo hivyo!” 89:16-17

Bi maana mambo hayako namna hiyo. Allaah (Ta´ala) anawapa mtihani waja Wake kwa utajiri na ufakiri ili kuona ni nani ambaye ni mpambanaji, mwenye kushukuru na mwenye kusubiri. Kama ambavyo anawapa mtihani waja Wake kwa misiba na maradhi ili kuwasafisha kutokamana na madhambi na maasi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 143
  • Imechapishwa: 01/11/2016