62. Ni vita vipi vilivyotokea mwaka wa tisa?

Swali 62: Ni vita vipi vilivyotokea mwaka wa tisa?

Jibu: Katika Rajab kulitokea vita vya Tabuuk, ambavyo pia viliitwa “vita vya ´Usrah”. Wakati wa vita hivi ‘Uthmaan bin Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) alitayarisha ngamia 300 waliobeba mizigo kamili, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamteua Aliy bin ´Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ́anh) kuwa naibu wa Madiynah. Hapa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifunga mkataba wa amani na Aylah, Adhruh na Ukaydir Duumah. Akarudi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyumbani baada ya kukaa Tabuuk kwa muda wa siku ishirini. Walipokuwa njiani wakirudi nyumbani ndipo walipofedheheshwa wanafiki ambapo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akateremsha:

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

“Wanaapa kwa Jina la Allaah kwamba hawakusema [neno la kufuru] na hali wamekwishasema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.”[1]

Katika mwaka huohuo ndio ulijengwa msikiti wa Dhwiraar na Allaah akawasamehe wale wanaume watatu waliobaki nyumbani: Ka´b bin Maalik, Muraarah bin ar-Rabiy′ na Hilaal bin Umayyah. Hakuna wanaume wengine waliokuwa na uwezo waliobaki nyuma isipokuwa wale waliokuwa na udhuru.

[1] 09:74

  • Mhusika: ´Allaamah Haafidhw bin Ahmad al-Hakamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Amaaliy fiys-Siyrah an-Nabawiyyah, uk. 126
  • Imechapishwa: 28/10/2023