3 – Ya´juuj na Ma´juuj. Ni majina mawili ya kiajemi au ya kiarabu yaliyochukuliwa kutoka katika (المأج) ambako ni kutikisika au kuwashwa moto na kuwaka kwake. Wawili hao ni viumbe wawili wa kibinadamu wanaopatikana kwa dalili ya Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema katika kisa cha Dhul-Qarnayn:

حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ بَيْنَ السَّدَّيْنِ وَجَدَ مِن دُونِهِمَا قَوْمًا لَّا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ قَوْلًا قَالُوا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِنَّ يَأْجُوجَ وَمَأْجُوجَ مُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ فَهَلْ نَجْعَلُ لَكَ خَرْجًا عَلَىٰ أَن تَجْعَلَ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ سَدًّا

“Hata alipofikia kati ya milima miwili akakuta nyuma yake watu ambao wanakaribia kutofahamu neno lolote. Wakasema: Ee Dhul-Qarnayn! Hakika Ya´juuj na Ma´juuj wanaeneza ufisadi katika ardhi. Basi ,je, tukufanyie ujira ili uweke kati yetu na kati yao kizuizi?”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee Aadam! Simama na upeleke kundi la moto katika wana wako.” mpaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema: “Furahini! Kwani hakika katika nyinyi kuna mmoja na katika Ya´juuj na Ma´juuj kuna elfumoja.”[2]

Wameipokea katika “as-Swahiyh” mbili.

Kujitokeza kwao, ambako ni moja katika alama za Qiyaamah bado haijajitokeza, lakini mwanzo wake umepatikana katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Leo kumefunguliwa katika ile tundu ya Ya´juuj na Ma´juuj kama hivi – na akaonyesha kidole gumba na kidole kinachofuata.”[3]

Kujitokeza kwao kumethibiti kwa Qur-aan na Sunnah.

Allaah (Ta´ala) amesema:

حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ وَاقْتَرَبَ الْوَعْدُ الْحَقُّ

“Mpaka watakapofunguliwa Ya´juuj na Ma´juuj nao kutoka kila mwinuko watateremka. Na itakaribia ahadi ya haki [Qiyaamah].”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Qiyaamah hakitosimama mpaka muone kabla yake alama kumi… “ ambapo akataja moto, ad-Dajjaal, mnyama, kuchomoza jua kutoka upande wa magharibi na kuzama kwake upande wa mashariki, kushuka kwa ´Iysaa mwana wa Maryam, Ya´juuj na Ma´juuj na khusuuf tatu; Khasf yenye kutoka upande wa mashariki, khasf kutoka upande wa magharibi, khasf kutoka katika kisiwa cha kiarabu na mwisho [wa alama hizo] ni moto utaotokea upande wa magharibi ambao utawafukuza kwenda katika uwanja wa mkusanyiko.”[5]

Ameipokea Muslim.

Kisa chao kiko katika Hadiyth ya an-Nawwaas bin Sam´aan ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu ´Iysaa mwana wa Maryam baada ya kumuua kwake ad-Dajjaal:

“Wakati atapokuwa katika hali hiyo ndipo Allaah atamfunulia Wahy ´Iysaa kwamba Mimi nimewatoa waja Wangu hatodhalilishwa yeyote kwa kuwaua hao. Wahifadhi waja wangu kwenda katika [mlima wa] at-Twuur na Allaah atamfufua Ya´juuj na Ma´juuj na watakuwa ni wenye kushuka katika kila jibali. Wale wa mwanzo wao watapita katika bahari ya at-Twabariyyah ambapo wanywe maji yake yote. Watapita wa mwisho wao na waseme “hapa kulikuweko maji mara fulani”. Kisha wataondoka zao mpaka wafike katika mlima wa Khamr ambao ni mlima wa Yerusalemu na waseme: “Tumewaua walioko ardhini. Kwa hiyo njooni tuwaue walioko juu mbinguni”. Kwa hiyo warushe ile mishale yao mbinguni na Allaah awarudishie mishale yao hali ya kutapakazwa damu. Mtume wa Allaah na wafuasi wake watawadhibiti mpaka kichwa cha fahali kwa mmoja wao kiwe bora kuliko vipande vya dhahabu mia moja kwa mmoja wenu hii leo. Mtume wa Allaah na wafuasi wake waelekee kwa Allaah. Allaah atawapelekea wadudu katika shingo zao. Matokeo yake waanguke kama kifo cha nafsi moja. Kisha Mtume wa Allaah na wafuasi wake washuke ardhini na hawatopata maeneo pa shibri moja isipokuwa wamejazwa na mizoga na harufu yao mbaya. Mtume wa Allaah na wafuasi wake waelekee tena kwa Allaah. Ndipo Allaah atawapelekea ndege kama shingo za ngamia. Watawabeba na wawatupe pale atakapotaka Allaah.”[6]

Ameipokea Muslim.

[1] 18:93-94

[2] al-Bukhaariy (6530) na Muslim (222, 379).

[3] al-Bukhaariy (7135) na Muslim (2880, 02).

[4] 21:96-97

[5] Muslim (2901, 39).

[6] Muslim (2937, 110). Rejea maelezo ya an-Nawawiy juu ya ugeni wa Hadiyth katika “Riyaadh-us-Swaalihiyn” (1817).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 108-109
  • Imechapishwa: 13/11/2022