2 – Kuteremka kwa ´Iysaa mwana wa Maryam. Kushuka kwa ´Iysaa mwana wa Maryam ni jambo limethibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ

“Hakuna yeyote katika Ahl-ul-Kitaa isipokuwa atamwamini kabla ya kufa kwake.”[1]

Bi maana kufa kwa ´Iysaa. Haya yatatokea wakati ataposhuka. Hivo ndivo alivyofasiri Abu Hurayrah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Naapa kwa Allaah atashuka ´Iysaa mwana wa Maryam hali ya kuwa ni mwamuzi na mwadilifu.”[2]

Kuna maafikiano juu ya Hadiyth hii.

Waislamu wameafikiana juu ya kushuka kwake ambapo atashuka kwenye mnara mweupe mashariki mwa Dameski hali ya kuwa ameweka viganja vyake vya mikono juu ya mbawa za Malaika wawili. Hatashuka kwa kafiri yoyote atakayepata harufu ya pumzi zake isipokuwa atakufa. Pumzi zake zinafikia mwisho wa yanapofika macho yake. Atamtafuta ad-Dajjaal mpaka ampate katika mlango wa al-Ludd ambapo amuue, atavunja msalaba, ataondosha kodi na atasujudiwa Mmoja ambaye ni Allaah, Mola wa walimwengu. Aidha atahiji na kufanya ´umrah. Yote haya yamesihi katika “as-Swahiyh” ya Muslim na mengine yako kwa wote wawili al-Bukhaariy na Muslim[3]. Imaam Ahmad na Abu Daawuud wamepokea:

“´Iysaa baada ya kumuua ad-Dajjaal atabaki miaka arobaini kisha atakufa na waislamu watamswalia.”[4]

al-Bukhaariy ametaja katika kitabu chake “Taariykh” kwamba atazikwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[5].

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] 04:159

[2] al-Bukhaariy (2222) na Muslim (155, 242).

[3] Rejea Hadiyth ya an-Nawwaas bin Sam´aan ilioko kwa Muslim (2937, 110, 111).

[4] Ahmad (9259), Abu Daawuud (4324), Ibn Hibbaan (08/277) na al-Haakim (02/595) ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Ameipokea vilevile Ibn Abiy Shaybah (15/158) na Ibn Jariyr (09/388). Shaykh Ahmad Shaakir amesahihisha cheni ya wapokezi wake katika maelezo yake ya al-Musnad.

[5] al-Bukhaariy katika ”Taariyk-ul-Kabiyr” (01/263), at-Tirmidhiy (3617), al-Aajurriy katika ”ash-Shariy´ah” (381) kupitia kwa ´Uthmaan bin adh-Dhwahhaak, kutoka kwa Muhammad bin Yuuusuf bin ´Abdillaah bin Salaam, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake ambaye amesema:

”Ndani ya Tawraat kumeandikwa sifa za Muhammad na sifa za ´Iysaa mwana wa Maryam kwamba watazikwa pamoja.”

al-Bukhaariy amesema:

”Naona kuwa si yenye kusihi na wala hayafuatwi.”

at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth hii ni nzuri na geni.”

al-Haythamiy amesema katika ”al-Jaamiy´” (08/306):

”Katika cheni ya wapokezi yuko ´Uthmaan bin adh-Dhwahhaak ambaye Ibn Hibbaan amesema kuwa ni mwaminifu lakini amedhoofishwa na Abu Daawuud.”

al-Haafidhw amesema katika ”al-Fath” (07/66):

”Amepokea kutoka kwake – bi maana ´Aaishah – katika Hadiyth isiyothibitisha alimwomba idhini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba akiisihi baada yake azikwe pembezoni mwake. Akamwambia ´Aaishah: “Ni vipi nitakufanyia jambo hilo? Maeneo hapo hakuna isipokuwa kaburi langu, kaburi la Abu Bakr, ´Umar na ´Iysaa mwana wa Maryam.”

Imekuja katika khabari za Madiynah kupitia njia dhaifu kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab ambaye amesema:

“Makaburi ya watu watatu yamo nyumbani mwa ´Aaishah. Kuna sehemu ya kaburi ambapo atazikwa ´Iysaa bin Maryam.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 106-107
  • Imechapishwa: 13/11/2022