62. Adabu ya pili iliyopendekezwa: Kuharakisha kukata swawm

Miongoni mwa adabu za funga zilizopendekezwa na kuharakisha kukata swawm inapohakikika kuzama kwa jua kwa kuliona kwa macho au ukawa na dhana yenye nguvu kwamba limekwishazama kwa taarifa yenye uhakika kwa njia ya adhaana au nyengine. Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyopokea kutoka kwa Mola Wake (´Azza wa Jall):

“Hakika waja Wangu wanaopendwa zaidi kwangu ni wale wanaoharakisha kufutari.”[1]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy.

Sunnah ni mtu akate swawm kwa tende tosa. Akizikosa basi akate swawm kwa tende za kawaida na akikosa basi akate swawm kwa maji. Hayo ni kutokana na maneno ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifutari kabla ya hajaswali kwa tende tosa. Isipokuwa tende tosa basi tende za kawaida. Isipokuwa tende za kawaida basi kwa funda la maji.”

Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy[2].

Asipopata tende tosa, tende za kawaida wala maji basi akate swawm kwa kile chakula au kinywaji kitachokuwa chepesi kwake na halali. Asipopata kitu basi anuie kukata swawm kwa moyo wake. Asijiweke vidole vyake au akakusanya mate kisha akayameza kama wanavofanya baadhi ya watu wajinga.

Mfungaji anatakiwa kuomba du´aa kwa yale anayoyapenda. Ibn Maajah amepokea katika “as-Sunan” yake kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mfungaji wakati wa kufutari kwake ana du´aa isiyorudishwa nyuma.”

Amesema katika “az-Zawaa-id”:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”[3]

Abu Daawuud amepokea kutoka kwa Mu´aadh bin Zahrah Mursal kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anapokata swawm anasema:

اللَّهُمَّ لَكَ صُمْتُ وَعَلَى رِزْقِكَ أَفْطَرْتُ

“Ee Allaah! Nimefunga kwa ajili yako na nimefutari kwa riziki yako.”[4]

Abu Daawuud amepokea tena kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapofutari basi husema:

ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتِ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الْأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ

“Kiu kimeondoka, mishipa imerowana na ujira umepatikana – Allaah akitaka.”[5]

[1] Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. al-Mundhiriy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na geni.”

[2] Cheni ya wapokezi ni nzuri sana.

[3] Baadhi yao wameidhoofisha. Sababu ya kutofautiana kwao ni juu ya usahihi wake na kutofautiana kwao juu ya kulengesha moja ya mapokezi yake. Lakini hata hivyo inayo shawahidi katika kuitikiwa du´aa ya mfungaji katika hali ya kuachia. Kwa hiyo Hadiyth inakuwa nzuri.

[4] Mu´aadh bin Zahrah ni Taabiy´. Ibn Hibbaan amemfanya kuwa mwaminifu. Hadiyth ni dhaifu ambayo katika cheni ya wapokezi wake kuna Swahabah anayekosekana. Lakini inatolewa ushahidi na nyengine pengine ikaitilia nguvu.

[5] Cheni ya wapokezi ni nzuri.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 26/04/2021