Swali 61: Ulinganizi juu ya mfumo wa Salaf umeenea. Lakini wako wanaosema kuwa ulinganizi huu unagawanya, kuwatawanyisha na kuwafanya waislamu wao kwa wao kugongana ambapo wanashughulikiana badala ya adui yao wa kweli. Je, haya ni kweli?

Jibu: Huku ni kuyageuza mambo. Kulingania katika Tawhiyd na mfumo wa Salaf kunaleta umoja. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane!”[1]

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja Nami ni Mola wenu, basi niabuduni!”[2]

Waislamu hawawezi wakawa na umoja isipokuwa juu ya Tawhiyd na mfumo wa Salaf. Wakiiruhusu mifumo inayopingana na mfumo wa Salaf ndipo watafarikiana na kugawanyika. Mambo yako namna hiyo hii leo. Ambaye analingania katika Tawhiyd na mfumo wa Salaf ndiye ambaye analingania katika umoja. Ambaye analingania katika mambo mengine ndiye ambaye analingania katika mfarakano na tofauti[3].

[1] 3:103

[2] 21:92

[3] Kwa mujibu wa mapote kama vile Jamaa´at-ut-Tabliygh na al-Ikhwaan al-Muslimuun kulingania katika Tawhiyd kunawaganya waislamu. Hawaoni kulingania katika Tawhiyd ni katika msingi yao. Hawako radhi juu ya watu wanaolingania katika Tawhiyd. Pindi mtu anapojiunga nao wanamtahadharisha kuongelea Tawhiyd. Haya yamemtokea Muhammad bin ´Abdillaah bin Muhammad al-Ahmad, kama alivosema Shaykh Hamuud at-Tuwayjiriy (Rahimahu Allaah):

”Baada ya ´Aswr kiongozi (kiongozi wa Jamaa´at-ut-Tabliygh) amenitaka kuwakhutubia neno mahujaji. Kwa vile nilikuwa bado mpya ndani ya kundi hili kiongozi akamwomba msaidizi wake kunielekeza kwanza. Msaidizi yula akasema: ”Utapokuwa unaongea basi unalazimika kujiepusha na mambo matatu ikiwa ni pamoja na shirki na Bid´ah. Sababu iliyofanya ulinganizi wa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab kufupika ni kutilia mkazo wa zaidi katika jambo hilo.” (al-Qawl al-Baliygh fiyt-Tahdhiyr min Jamaa´at-it-Tabliygh, uk. 46)

Kuna mifano mingi kabisa juu ya hilo. Rejea katika kitabu kilichotajwa basi utajionea maajabu makubwa kabisa.

Kuhusu al-Ikhwaan al-Muslimuun, ni kikundi ambacho hamu yake kubwa ni kukusanya tu. Wanawakusanya Ahl-ul-Bid´ah wal-Ahwaa´ wote. Raafidhwah ni ndugu zao. Jahmiyyah, Mu´tazilah, Khawaarij, washerekeaji wa maulidi, waabudia makaburi na Suufiyyah ni ndugu zao pia. Bali mpaka mayahudi na manaswara pia! Hapa kunakuja baadhi ya mifano juu ya hilo: Hasan al-Bannaa amesema:

”Ugomvi wetu na mayahudi sio kwa kidin. Kwa sababu Qur-aan tukufu imekokoteza juu ya kuwaonyesha ukarimu na urafiki.”

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) aliulizwa juu ya maneno hayo ambapo akajibu:

”Maneno haya ni batili na machafu. Mayahudi ni miongoni mwa maadui wakubwa kwa waumini na watu waovu kabisa. Bali wao ndio watu wenye uadui mkubwa kwa waumini. Kwa hivyo maneno haya ni ya kimakosa, ya kidhuluma, mabaya na ya kiovu.”

Amesema tena (Rahimahu Allaah):

”Ni ukafiri na kuritadi akisema kuwa hakuna kitu kati ya Uislamu na mayahudi.” (al-´Awaaswim mimmaa fiy Kutub Sayyiq Qutwub min al-Qawaaswim, uk. 65-66)

Kuhusu manaswara Dr Hassaan Hathuut wa kipote hicho amesema:

”Mwanzoni kulikuwa na umati mkubwa wa watu wakiongozwa na wanazuoni wa Kiislamu na makasisi wa coptic. Kulikuwa na mapenzi, uchangamfu na udugu.

Kwa mnasaba wa kuzungumzwa makasisi wa coptic, watu wengi wanajaribu kumtuhumu bwana huyo (bi maana Hasan al-Bannaa) kuwa na chuki dhidi ya manaswara au uchochezi wa mgawanyiko nchini. Allaah na wale wahudhuriaji katika wakweli wanashuhudia ya kuwa kinyume chake ndio sahihi.

Bwana huyo hakuwa akilingania katika chuki na mfarakano. Alikuwa akithibitisha kuwa ulinganizi kwa kutekeleza Shari´ah ya Kiislamu hauwezi kuelekezwa kwa wale wakopti. Kwa sababu Shari´ah ingelitumika juu yetu sisi na wao, pili isingeliteka ukristo wa wakristo. Shari´ah si vyengine isipokuwa ni mkusanyiko wa kanuni ambazo hakuna mfano wake katika unaswara na wala ambayo haipingani na hukumu za unaswara. Ikiwa kuna tofauti zozote, manaswara wangeendelea kuhukumu kulingana na Injiyl. Uislamu hauna tatizo lolote juu ya hilo. Muda wa kuwa maoni ya wengi hayapingani na maoni ya wachache, basi hakuna mwenye kudhulumu wala mwenye kudhulumiwa.

Ulinganizi wa bwana huyo ulipata waislamu wenye busara na wakopti. Inatosha katika kujibu tuhuma zinazosema kuwa alikuwa na chuki dhidi ya manaswara kwamba Louis Fanous, ambaye alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa wakopti, alikuwa ni mmoja katika wasikilizaji wa mara kwa mara wa darsa analolitoa Hasan al-Bannaa. Wakati Hasan al-Bannaa alipogombea ubunge, naibu wake katika uchaguzi huo alikuwa mkopti. Wakati Hasan al-Bannaa alipouliwa na serikali ikapiga marufuku kusindikiza jeneza lake, hakuna waliotembea nyuma ya machela yake isipokuwa tu watu wawili: baba yake na ´Ubayd az-Zaa´iym ambaye ni mkristo na mwanasiasa. Nakumbuka wakati tulipokuwa wanafunzi tulikuwa tukizitembelea jumuiya za kinaswara ili kuzungumzia msimamo wa Uislamu juu ya ukristo. Hakika tulihisi kuwa ndio watu walio karibu zaidi na sisi kimapenzi.” (Hasan al-Bannaa bi Aqlaam Talaamidhatih wa Mu´aaswirih, uk. 188)

Hakuna haja ya maelezo. Yako wazi. Natosheka na nukuu hii ijapo ni ndefu. Nilichokuwa nataka watu kufahamu ni kwamba msingi wa al-Ikhwaan al-Muslimuun ni kuwasanya watu kwa kutumia jina la Uislamu pasi na kutilia umuhimu kuzisahihisha ´Aqiydah. Kwa sababu kulingania katika Tawhiyd na mfumo wa Salaf hauwafikishi katika kufanya urafiki na mayahudi, manaswara, Raafidhwah na Ahl-ul-Bid´ah wal-Ahwaa´ ambao ni wapotofu na wanapotosha. Msingi wao ni nukuu ya Hasan al-Bannaa inayotambulika. Dr Hassaan Hathuut amesema:

”Miongoni mwa mafunzo yake profesa al-Bannaa ambayo aliyakariri mara nyingi pasi na kuchoka ni maneno yake yanayotambulika ambayo bado yako hai mpaka hii leo:

”Tunatekeleza kwa pamoja yale tunayoafikiana kwayo na tunapeana udhuru kwa yale tunayotofautiana kwayo.” (Hasan al-Bannaa bi Aqlaam Talaamidhatih wa Mu´aaswirih, uk. 190)

Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ndio, ni wajibu kushirikiana katika yale tunayoafikiana, kwa ajili ya kuinusuru haki, kuitilia umuhimu na kutahadharisha juu ya yale ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamekataza. Ama kuhusu kupeana udhuru katika yale tunayotofautiana, si moja kwa moja hivo. Suala hili linahitaji upambanuzi; ikiwa ni katika yale mambo ya Ijtihaad ambayo dalili yake imefichikana, basi ni wajibu kutokukemeana sisi kwa sisi. Kuhusu yale yanayopingana na dalili ya Qur-aan na Sunnah, basi ni lazima kumkemea yule anayeenda kinyume na dalili kwa hekima, maneno mazuri na mahojiano mazuri.” (Tanbiyhaat Haammah ´alaa maa katabahu ash-Shaykh Muhammad ´Aliy as-Swaabuuniy fiy Swifaatillaah (´Azza wa Jall), uk. 18-19)

Maneno haya yaliyoachiwa yako wazi kabisa kwamba yanapingana na kanuni ya kupenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah. Msingi wake ni kanuni ya bwana wa gazeti la ”al-Manaar”. Baada ya hapo yakahamia kwa al-Ikhwaan al-Muslimuun kwa sababu yameafikiana na matamanio ya nafsi zao:

Yamenijia matamanio yake kabla ya mimi kujua ni nini matamanio

yakaja katika moyo mtupu na hivyo yakakita

Shaykh Bakr Abu Zayd (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu nukuu inayotambulika ya al-Ikhwaan al-Muslimuun:

”Shida hii imezuliwa na haiko salama. Ambaye anaenda kinyume na hukumu za Kiislamu za kukata kabisa hapewi udhuru wowote. Waislamu wameafikiana juu ya kwamba haifai kutoa udhuru wala kupakana mafuta juu ya misingi ya ´Aqiydah. Ni mapote mangapi yanayotupilia mbali misingi iliyowekwa katika Shari´ah na yakabishana juu yake kwa batili!”(Hukm-ul-Intimaa’, uk. 149)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 163-167
  • Imechapishwa: 27/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy