Swali 60: Ni vipi watawala wanatakiwa kheri?

Jibu: Hilo linakuwa kwa njia mbambali:

1 – Kuwaombea du´aa ya kurekebika na kunyooka. Kwa sababu ni katika Sunnah kuwaombea du´aa watawala wa waislamu, khaswa katika zile nyakati na yale maeneo ambayo kuna matarajio makubwa ya kuitikiwa du´aa[1]. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

”Lau ningelijua kuwa nina du´aa inayoitikiwa basi ningemwombea nayo mtawala.”[2]

Akitengemaa mtawala basi jamii nzima inatengemaa na akiharibika mtawala basi jamii nzima inaharibika.

2 – Kuzitekeleza zile kazi wanazowapa wafanyikazi.

3 – Wazinduliwe juu ya makosa na maovu ambayo yanakuwepo katika jamii na ambayo pengine hawayajui. Hata hivyo uzindushi huo unakuwa kwa siri[3]. Nasaha haiwi kwa njia ya kuanikwa mbele ya watu au juu ya mimbari. Kwa sababu sababu mfumo huo unachochea shari na chuki kati ya watawala na raia.

Sio katika kuwatakia kheri mtu akayazungumza makosa ya watawala juu ya mimbari au mbele ya watu. Hili halileti manufaa. Hili linazidisha shari juu ya shari[4]. Kuwatakia mema ni kuwasiliana moja kwa moja na mtawala[5], kwa njia ya uandishi au kumtumia mjumbe ambaye atamfikishia nasaha zako baina yako wewe na wao.

Wala sio katika kuwatakia mema tukaandika nasaha na kusambaza hadharani ili kila mtu aisome. Hiyo sio nasaha, hiyo ni fedheha. Haya ni miongoni mwa mambo yanayosababisha shari, kuwafurahisha maadui na kuwachochea watu wa matamanio.

[1] Imaam Abu Muhammad al-Hasan bin ´Aliy al-Barbahaariy amesema:

”Ukimuona mtu anaomba du´aa dhidi ya mtawala, basi tambua kuwa ni mtu anayefuata matamanio. Ukimuona mtu anamuombea mtawala du´aa ya kutengemaa, basi tambua kuwa ni mtu wa Sunnah – Allaah akitaka.” (Sharh-us-Sunnah, uk. 116)

Salaf wana mapokezi mengi wakimuombea mtawala ni mengi.

al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

”Lau ningelikuwa na du´aa inayojibiwa, basi nisingemwombea mwingine isipokuwa kiongozi.” Akaambiwa: ”Kwa nini hivo, ee Abu ´Aliy?” Akasema: ”Ningejiombea mwenyewe, basi ingenifaa mimi peke yangu. Lakini ningemwombea mtawala, basi kutengemaa kwa mtawala ndio kutengemaa kwa waja na miji.” (Abu Nu´aym (8/91) na al-Khallaal (9))

Imaam Ahmad alisema kumwambia mwanawe ´Abdullaah:

”Namuomba Allaah (´Azza wa Jall) arefushe umri wa kiongozi wa waumini, amthibitishe na amsaidie kwa msaada Wake. Kwani hakika Yeye juu ya kila jambo ni muweza.” (as-Sunnah (1/140) ya ´Abdullaah bin Ahmad)

[2] Majmuu´-ul-Fataawaa (28/391) na Kashshaf-ul-Qinaa´ (2/37).

[3] Hii ndio njia bora kabisa katika kuwanasihi watawala. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametufunza nayo pale aliposema:

”Yeyote ambaye yuko na nasaha kwa mtawala basi asiseme hadharani. Badala yake amshike mkono wake na akae naye chemba. Akikubali amekubali na vinginevyo ametekeleza jukumu lake na haki yake.”

[4] Kunasihi hadharani kuna madhara mengi:

1 – Ni aina fulani ya kujionyesha na kutaka kuonekana. Hakika inatambulika ile shari inayopatikana kwa ajili ya kujionyesha katika kuharibika kitendo chake. Kitendo kinapokuwa kimejificha basi kuna matarajio makubwa kwa Allaah kukikubali.

2 – Kuna matarajio makubwa kwa yule mwenye kunasihiwa kutokukubali, kwa sababu huona kuwa ni fedheha na sio nasaha. Isitoshe kiburi kinaweza kumfanya akatenda dhambi, ambapo yule aliyenasihi anakuwa na fungu lake fulani la madhambi.

3 – Ingawa kuwakosoa watawala hadharani si sahihi, kunaichochea pia jamii nzima na kuwajaza chuki wananchi dhidi ya watawala. Inaweza vilevile kupelekea wato kutotiiwa katika yaliyo mema – na huu ndio mwenendo wa Khawaarij.

Kuuliwa kwa ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) hakukutokana na sababu nyingine isipokuwa yale yaliyofanywa na baadhi ya wajinga juu ya Sunnah na wakawafuata na wakawafuata wachochezi ambao walikuwa wakiwapa watu mchanga wa machoni kuhusiana na khaliyfah mwongofu ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh).

[5] Kama wanavofanya wanazuoni.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 161-163
  • Imechapishwa: 27/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy