59. Ni vipi vijana chipukizi watatangamana na wazushi na watu wenye fikira za kubomoa na ´Aqiydah potofu?

Swali 59: Ni vipi vijana chipukizi watatangamana na wazushi na watu wenye fikira za kubomoa na ´Aqiydah potofu?

Jibu: Vijana wanapaswa kujiepusha na wazushi na watu wenye mifumo ya kuharibu na fikira potofu. Wanatakiwa kujiepusha nao na vitabu vyao. Sambamba na hilo walazimiane na wanazuoni na watu wenye utambuzi na watu wenye ´Aqiydah iliyosalimika. Wachukue elimu kutoka kwao. Waketi nao na wawaulize wao.

Kuhusu wazushi na watu wenye fikira za kubomoa, ni lazima kwa vijana kujitenga nao mbali. Kwa sababu watawafanyia mabaya. Watawapandikiza ´Aqiydah mbovu, Bid´ah na mambo ya ukhurafi. Jengine ni kwamba mwalimu anakuwa na athari kwa mwanafunzi. Kijana hupotea kwa sababu ya mwalimu mpotevu. Sambamba na hilo wanafunzi na vijana hunyooka wakiwa na mwalimu mzuri. Mwalimu analo jukumu kubwa. Kwa hivyo tusilichukulie wepesi jambo hili[1].

[1] Allaah amlipe Shaykh wetu malipo mazuri! Amewabainishia vijana mfumo wa Salaf katika kutangamana na wazushi. Wao na vitabu vyao wote wanatakiwa kuepukwa. Endapo Shaykh wetu angesema kuwa tunachukua yale mazuri walionayo na kuyaacha yale mabaya walionayo, kama wanavonadi watu wa mfumo wa haki sawa hii leo, basi vijana wangelipotea, mfumo wa Salaf ungeliyeyuka na kulegea na ´Aqiydah za vizazi vinavyokuja huko mbele zingelichafuka.

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amefanya katika kila zama na kila pahali watu wanaotetea na kubainisha na kuuweka wazi mfumo wa Salaf, ijapo watachukia wale wahalifu! Rejea jawabu la Shaykh juu ya swali la 19.

al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hakika mambo yalivyo kuna wanazuoni wawili tu: mwanachuoni wa dunia na mwanachuoni wa Aakhirah. Mwanachuoni wa dunia elimu yake ni yenye kuenezwa. Mwanachuoni wa Aakhirah elimu yake ni yenye kufichwa. Mfuate mwanachuoni wa Aakhirah na achana na mwanachuoni wa dunia. Asikuzuieni kwa kilevi chake.” (Hilyat-ul-Awliyaa’ (8/92))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 160
  • Imechapishwa: 27/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy