61. Je, imesuniwa Sujuud ya kusahau katika hali hizi tatu?

Swali 61: Je, Sujuud ya kusahua imesuniwa katika maeneo yafuatayo:

1 – Akisoma katika zile Rak´ah mbili za mwisho baada ya al-Faatihah kile kitachomsahilikia kutoka katika Qur-aan?

2 – Akisoma katika Sujuud yake au akasema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

kwa mfano kati sijda mbili?

3 – Akisoma kwa sauti ya juu katika swalah za kusoma kimyakimya au akasoma kimyakimya katika swalah za kusoma kwa sauti ya juu?

Jibu: Akisoma katika Rak´ah mbili za mwisho swalah ya Rak´ah nne au moja wapo baadhi ya Aayah hali ya kusahau haikusuniwa kwake kusujudu. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayofahamisha kusoma baada ya al-Faatihah katika Rak´ah ya tatu na Rak´ah ya nne ya Dhuhr. Vilevile imethibiti ya kwamba alimsifu kiongozi ambaye alikuwa akisoma katika Rak´ah zote za swalah zake baada ya al-Faatihah:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ

“Sema: ”Allaah ni Mmoja pekee.”[1]

Lakini kinachojulikana kutoka kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwamba alikuwa hasomi katika Rak´ah ya tatu na Rak´ah ya nne isipokuwa al-Faatihah peke yake. Hayo yamepokelewa na al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh).

Vilevile imethibiti kutoka kwa as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) kuwa alisoma katika Rak´ah ya tatu ya swalah ya Maghrib baada ya al-Faatihah:

رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا

“Mola wetu usizipotoe nyoyo zetu baada ya kutuongoza.”[2]

Yote hayo yamefahamisha juu ya wasaa wa jambo hili.

Kuhusu ambaye atasoma katika Rukuu´ au Sujuud hali ya kusahau basi atasujudu sijda ya kusahau. Haijuzu kwake kukusudia kusoma katika Rukuu´ na Sujuud. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza jambo hilo. Kwa hivyo akisoma kwa kusahau kwenye Rukuu´ au Sujuud, basi analazimika kusujudu sijda ya kusahau. Vivyo hivyo mwenye kusahau katika Rukuu´ ambapo akasema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola wangu Aliye juu.”

badala ya:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

au akasahau katika Sujuud ambapo akasema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

badala ya:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika Mola wangu Aliye juu.”

basi analazimika kusujudu kwa sababu ameacha jambo la wajibu kwa kusahau. Akiwa amekusanya kati ya hayo mawili katika Rukuu´ hali ya kusahau, basi haimuwajibikii kusujudu. Lakini akisujudu kwa kusahua haina neno kutokana na kuenea kwa dalili. Hili ni kwa imamu, anayeswali peke yake na ambaye amejiunga na imamu baada ya kuchelewa sehemu ya swalah. Kuhusu mswaliji ambaye alikuwa pamoja na imamu kuanzia mwanzo wa swalah hahitaji kufanya Sujuud ya kusahau katika maeneo haya. Analazimika kumfata imamu wake. Vivyo hivyo akisoma kwa sauti ya juu katika zile swalah za kusoma kimyakimya au kinyume chake haitomlazimu kusujudu. Kwa sababu baadhi ya wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwasikilizisha baadhi ya Aayah katika swalah za kusoma kimyakimya.

[1] 112:01

[2] 03:08

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 12/09/2022