61. Dalili juu ya kwamba kutulia na kupangilia ni nguzo

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah kuhusiana na mtu aliyekuwa akiswali vibaya. Kasema:

“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuliingia mtu, akaswali kisha akamsalimia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamwambia “Rudi ukaswali, hakika hujaswali.” Alifanya hivi mara tatu. Mwishoni akamwambia: “Naapa kwa yule aliyekutuma kwa haki; siwezi bora zaidi ya hivi. Nifunze!” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Unaposimama kutaka kuswali, lete Takbiyr. Kisha soma uwezacho katika Qur-aan. Kisha utarukuu mpaka unyooke. Kisha utasimama sawa sawa. Kisha utasujudu mpaka utapotulia katika Sajdah. Kisha utainuka na kutulia katika kikao kisha utafanya hivyo katika swalah zote.”

MAELEZO

Dalili inayothibitisha kuwa kutulia katika matendo yote ya ´ibaadah na kupangilia kati ya nguzo ni nguzo ni Hadiyth ya yule bwana aliyeswali vibaya. Alidonoa swalah yake kama jogoo. Maneno yake:¨

“Rudi ukaswali, hakika hujaswali.”

Bi maana hujaswali swalah inayokubalika ki-Shari´ah ijapo aliswali swalah ilio na Rukuu´ na Sujuud kwa uinje wake. Akamkariria (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara tatu pengine atazinduka kosa lake. Sababu nyingine ya kumrudisha ni ili mafunzo yaweze kukita vizuri ndani ya moyo.

Hadiyth hii ni dalili inayojulisha kuwa kutulia ni nguzo katika matendo yote. Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwizi mbaya kabisa wa watu ni yule anayeiba katika swalah yake.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi ataiba katika swalah yake?” Akasema: ”Hatimizi Rukuu´ wala Sujuud yake.” au alisema: ”Hasimamishi swalah yake katika Rukuu´ na Sujuud.”[1]

Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

”Husemwa juu ya kila kitu kupunja.”[2]

Kupunja mizani. Maana yake ni kwamba Allaah akiwatishia maangamivu na adhabu wale wanaopunja mizani duniani, basi wale ambao wanapunja katika mizani ya dini ambapo wakazipunguza na kuzipunja swalah zao na wakazidonoa kama anavodonoa jogoo wanakuwa wabaya zaidi.

[1] Ahmad (05/310).  al-Haakim amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim ijapo hawakuipokea.” ”al-Mustadrak (01/353)).

[2] al-Muwattwa´ (01/12).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 24/01/2023