61. Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal ndio wenye kupinga uombezi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna wanaopinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallaam) isipokuwa Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal. Lakini haitokuwa isipokuwa baada ya idhini na kuridhiwa. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”[1]

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[2]

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

”Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye na akaridhia.”[3]

Haridhii isipokuwa Tawhiyd na wala haidhinishi isipokuwa wapwekeshaji. Washirikina hawana fungu lolote la uombezi. Amesema (Ta´ala):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi haitowafaa uombezi wowote wa waombezi.”[4]

MAELEZO

Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal ndio wanaopinga uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallaam). Kwa mfano Khawaarij na Mu´tazilah ambao wanawakufurisha watenda madhambi makubwa na wanasema kuwa watadumishwa Motoni milele na kwamba hautowafaa kitu uombezi wa waombezi.

Ama Ahl-us-Sunnah wanathibitisha uombezi. Lakini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallaam) na wengineo wenye kuombea hauwi isipokuwa kwa sharti mbili; Allaah amezitaja katika Qur-aan:

Sharti ya kwanza: Idhini ya Allaah kwa mwombezi aombee. Mambo si kama inavokuwa kwa watawala wa duniani ambao wanaombea mbele yake waombezi ijapokuwa hawakutoa idhini.

Sharti ya pili: Amridhie yule mwenye kuombewa awe miongoni mwa watu wenye kumwabudu Allaah pekee na katika waumini ingawa ana madhambi yanayomstahikisha kuingia Motoni au akaingia kwayo Motoni. Huyu ni muumini ambaye uombezi utamfaa kwa idhini ya Allaah.

Kuhusu kafiri uombezi hautomfaa isipokuwa yale yaliyobaguliwa katika uombezi wa Abu Twaalib, jambo ambalo ni maalum.

[1] 21:28

[2] 02:255

[3] 53:26

[4] 74:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 15/05/2021