60. Safari ya Mtume mbinguni kukutana na Mola wake

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Baada ya miaka kumi alipandishwa mbinguni… ”

Baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumaliza muda wa miaka kumi Makkah akiwalingania watu katika Tawhiyd alipandishwa mbinguni. Kwa msemo mwingine miaka mitatu kabla ya kuhajiri. Kuna maoni mengine yanasema mwaka mmoja kabla yake kutokana na makinzano ya wanazuoni. Mtunzi wa kitabu amechagua maoni yanayosema kuwa alipandishwa kabla ya miaka mitatu. Alipandishwa mbinguni baada ya kusafirishwa usiku kutokea Makkah kwenda Yerusalemu. Kwa sababu kwa mujibu wa maoni sahihi ni kwamba Israa´ na Mi´raaj yalipitika ndani ya usiku mmoja. Alisafirishwa wakati wa usiku kwa roho na kiwiliwili chake hali ya kuwa macho na si usingizini. Kuna maoni yanayosema kuwa alisafirishwa usiku akiwa usingizini. Yako maoni mengine yanayosema kuwa alisafirishwa usiku kwa roho yake. Kuna maoni mengine yanasema kuwa alisafirishwa usiku mara akiwa macho na mara nyingine akiwa usingizini. Maoni mengine yanasema kuwa kusafirishwa usiku ilikuwa katika usiku mmoja na kupandishwa mbinguni ilikuwa katika usiku mwingine.

Maoni sahihi ni kwamba kusafirishwa usiku na kupandishwa mbinguni ilikuwa katika usiku mmoja na wakati mmoja. Ilikuwa katika hali ya umacho na sio usingizini. Ilikuwa kwa roho na kiwiliwili. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa.”[1]

Mja ni neno limekusanya roho na kiwiliwili. Alipandishwa kwenda mbinguni baada ya kusafirishwa wakati wa usiku. Alisafirishwa kwa al-Buraaq kwa kusuhubiana na Jibriyl (´alayhis-Salaam). al-Buraaq ni mnyama mrefu kuliko punda na mdogo kuliko nyumbu. Mnyama huyo alimpanda Jibriyl (´alayhis-Salaam) na Muhammad (´alayhis-Swalaatu wa-Salaam) kutokea Makkah wakasafiri naye kwenda Yerusalemu Shaam. Hatua anayopiga al-Buraaq huyu ni umbali na upeo wa jicho. Kwa maana nyingine hatua moja anayopiga ni umbali wa mwisho wa jicho linaweza kuona. Katika kipindi hicho umbali kati ya Makkah na Shaam walikuwa wakienda mwezi mmoja kwa ngamia. Walikata masafa hayo kwa kipindi kifupi cha saa moja au saa na nusu. Ni takriban kama kasi ya ndege. al-Buraaq ameitwa hivo kwa sababu ana umeme na mwanga. Wakati walipofika Yerusalemu al-Buraaq akafungwa nje ya mlango na wakakusanyika Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaswalisha. Kisha kukaletwa Mi´raaj ikiwa kama ngazi, ambapo Jibriyl (´alayhis-Salaam) akapanda kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokea Yerusalemu kwenda juu mbinguni. Akapanda (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda katika mbingu ya chini ambapo akamkuta Aadam (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya pili ambapo akamkuta ´Iysaa (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya tatu ambapo akamkuta Idriys (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya nne ambapo akamkuta Yuusuf (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya tano ambapo akamkuta Haaruun (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya sita ambapo akamkuta Muusa (´alayhis-Salaam). Kisha akapanda kwenda katika mbingu ya saba ambapo akamkuta Ibraahiym (´alayhis-Salaam). Kila mbingu imehifadhiwa na iko na walinzi. Kila mbingu Jibriyl anaomba idhini ya kufunguliwa ambapo anaulizwa: “Ni nani?” Anajibu: “Jibriyl.” Anaulizwa tena: “Ni nani yuko pamoja nawe?” Anasema: “Muhammad.” Anaulizwa tena: “Ameitwa?” Anajibu: “Ndio.”

Kila mmoja katika Mitume alikuwa akimkaribisha na akikubali utume wake. Aadam alisema: “Karibu Nabii mwema na mwana mwema.” Ibraahiym alisema: “Karibu Nabii mwema na mwana mwema.” Mitume wengine walisema: “Karibu Nabii mwema na ndugu mwema.”

Kisha akavuka mkunazi baada ya mbingu saba mpaka akafika maeneo ambapo alisikia kalamu zikiandika ambapo Mola akamzungumzisha pasi na mkatikati. Hata hivyo kwa mujibu wa maoni sahihi hakumuona Allaah. Bali alimzumgumzisha nyuma ya pazia. Kuna maoni mengine yanayosema kuwa alimuona Allaah, maoni ambayo ni dhaifu. Maoni ya sawa ni kwamba alimuona kwa macho ya moyo wake na si kwa macho ya kichwani mwake. Kwa sababu hakuna yeyote awezaye kumuona Allaah duniani akiwemo Mtume pia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila anachoona katika uumbaji Wake[2].

Isitoshe wakati Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoomba kumuona:

قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا ۚ فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ

“Akasema: “(Lan) Hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.” Basi Mola wako alipojidhihirisha katika jabali akalifanya livurugike kuwa vumbi na Muusa akaanguka hali ya kuzimia. Alipozindukana akasema: “Utakasifu ni Wako! Nimetubu Kwako nami ni wa kwanza wa wanaoamini.””[3]

Kwa hivyo hakuna yeyote awezaye kumuona Allaah duniani. Kumuona Allaah ni miongoni mwa neema ambazo Allaah amewawekea nazo watu wa Peponi.

[1] 17:01

[2] Muslim (179).

[3] 07:143

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 95-97
  • Imechapishwa: 16/02/2023