6- Ambaye amezikwa kabla ya kuswaliwa au ameswaliwa na baadhi ya watu pasi na wengine. Inafaa kumswalia mtu huyo kaburini mwake kwa sharti imamu awe katika sura ya pili miongoni mwa wale watu ambao hawakumswalia. Kumepokewa Hadiyth zifuatazo juu ya hilo:

Ya kwanza: ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia:

“Kuna mtu mmoja alifariki – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimtembelea – wakamzika usiku. Kulipopambazuka wakamjuza. Akasema: “Ni kipi kilichokuzuieni kunijuza?” Wakasema: “Ilikuwa wakati wa usiku na kulikuwa na giza na tukachukia kukutia uzito. Akaliendea kaburi lake akamswalia. [Akatuongoza na tukapanga safu nyuma yake] [na mimi nilikuwa pamoja nao] [tukaleta Takbiyr nne].”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/91-92), Ibn Maajah (01/466) na mtiririko ni wake, Muslim (03/55-56) kwa mukhtasari. Pia ameipokea an-Nasaa´iy (01/284), at-Tirmidhiy (08/142), Ibn-ul-Jaaruud katika “al-Muntaqaa” (266), al-Bayhaqiy (03/45, 46), at-Twayaalisiy (2687), Ahmad (nambari. 1962, 2554, 3134) na ziada ya kwanza ni yao na ya al-Bukhaariy katika mapokezi yake (03/146, 147, 159). Ziada mbili za mwisho ni zake. al-Bayhaqiy, Muslim na an-Nasaa´iy wanazo ziada za mwisho.

Ya pili: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mwanamke mmoja mweusi alikuwa akifanya kazi [katika upokezi mwingine imekuja: “Akiokota vitambaratambara na miti] kutoka msikitini ambapo akafariki. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anamkosa. Baada ya siku kadhaa akamuulizia ambapo akaambiwa kwamba amefariki. Akasema: “Ni kwa nini hamkunijulisha?” [Wakasema: “Alifariki usiku ambapo akazikwa na hatukupendezwa kukuamsha.] [Ni kama kwamba walilidogesha jambo lake. Akasema: “Nielekezeni lililo kaburi lake ambapo wakamuonyesha. [Akaliendea kaburi lake ambapo akamswalia]. Kisha akasema: [“Thaabit akasema (ambaye ni mmoja wa wapokezi wa Hadiyth): “Wakati wa mazingira hayo au katika Hadiyth nyingine]: “Hakika makaburi haya yamejazwa giza kwa wakazi wake. Hakika Allaah (´Azza wa Jall) anawatilia nuru kwa mimi kuwaswalia.”

Ameitoa al-Bukhaariy (01/ 438, 439, 440 – 03/159), Muslim (03/56), Abu Daawuud (02/68), Ibn Maajah (01/465), al-Bayhaqiy (04/47) na mtiririko ni wake, at-Twayaalisiy (2446), Ahmad (02/352, 388, 406) kupitia kwa Thaabit bin Bunaaniy, kutoka kwa Abu Raafiy´ ambaye amepokea kutoka kwake.

Hakika nimependelea mtiririko huu niliyoutaja kwa sababu mpokezi wake hakuwa na mashaka juu ya kwamba maiti alikuwa ni mwanamke mweusi wakati ambapo kwa wengine mpokezi ametilia mashaka kama alikuwa ni mwanamke au mwanamme. Shaka imekuja kwa Thaabit au kwa Abu Raafiy´, kama alivyosisitiza al-Haafidhw Ibn Hajar. Upande wenye nguvu kwetu ni kwamba alikuwa mwanamke kutokana na njia zifuatazo:

1- Yakini ni yenye kutangulizwa mbele ya shaka.

2- Katika upokezi wa al-Bukhaariy imekuja kwa tamko:

“Mwanamke au mwanamme mmoja alikuwa akifanya kazi msikitini. Mimi sioni vyengine zaidi ya kwamba alikuwa mwanamke.”

Imekuwa na nguvu kwa mpokezi kwamba alikuwa mwanamke.

3- Hadiyth imepokelewa kwa njia nyingine tena kupitia kwa Abu Hurayrah ambapo mpokezi hakutilia mashaka. Tamko lake ni kama ifuatavyo:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkosa mwanamke mweusi ambaye alikuwa akiokota vitambaratambara na miti kutoka msikitini. Akasema: “Yuko wapi mwanamke fulani?” Wakasema: “Amefariki.”

Akaitaja Hadiyth namna hii. al-Bayhaqiy (02/440- 04/32) ameitaja kupitia kwa al-´Alaa´ bin ´Abdir-Rahmaan kutoka kwa baba yake ambaye amepokea kutoka kwake. Pia ameitaja Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” yake kama ilivyo katika “al-Fath”.

Ziada ya kwanza ni ya al-Bayhaqiy na Ibn Khuzaymah na nusu yake ya mwanzo ni ya Ahmad, ya pili ni ya Muslim na al-Bayhaqiy katika upokezi, pia ni ya al-Bukhaariy amepokea maana yake. Abu Daawuud na zile zilizotajwa mbili kwa Isnad nusu yake ya pili, ziada ya tatu ni ya al-Bayhaqiy na pia ya nne katika moja ya mapokezi yake. Vivyo hivyo ziada ya nne ni ya Muslim pia na Ahmad ambaye anayo ziada kutoka katika maneno ya Thaabit ilioko kwa al-Bayhaqiy pia.

al-Haafidhw ameupa nguvu upande huu kwa kumwigiliza al-Bayhaqiy ya kwamba ziada ya nne ni maneno ya mpokezi na si Hadiyth na kwamba ni katika Mursal ya Thaabit. Ibn-ut-Turkumaaniy amekwenda kinyume naye. Yeye ameona kuwa imetajwa kimlolongo kupitia kwa Abu Raafiy´ kutoka kwa Abu Hurayrah. Kwa sababu iko hivyo katika “as-Swahiyh” ya Muslim. Lakini hata hivyo maneno ya Thaabit haya yanasapotiwa na yale yaliyosemwa na wale wa mwanzo na inatilia nguvu kwamba Hadiyth imepokelewa katika upokezi wa Ibn ´Abbaas na ndani yake hamna ziada hii. Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (03/128/02).

Ni kweli kwamba ziada hii imethibiti au kwa maana kimlolongo katika Hadiyth nyingine ambayo ni iifuatayo:

Ya tatu: Yaziyd bin Thaabit – ambaye alikuwa ni mkubwa kuliko Zayd – amesema:

“[Siku moja] tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tulipofika al-Baqiy´ tahamaki akakutana na kaburi jipya ambapo akaliulizia. Wakasema: “Mwanamke fulani [ni mtumwa aliyeachwa huru wa Banuu fulani]. Akamtambua ambapo akasema: “Ni kwa nini hamkunijuza?” Wakasema: [Alikufa adhuhuri] wakati ambapo umejipumzisha usingizi wa mchana na umefunga ambapo hakutupendezwa kukuudhi. Akasema: “Msirudi kufanya hivo; nisipate tena tendo hili kwenu mara nyingine. Hatokufa miongoni mwenu yeyote atakayekufa muda wa kuwa niko nanyi isipokuwa mnapaswa mnijuze. Kwani hakika swalah yangu juu yake ni rehema. Kisha akaliendea kaburi hilo ambapo tukapanga safu nyuma yake. Akampigia Takbiyr nne.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (01/284), Ibn Maajah (01/465, 466), Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” (759- Mawaarid), al-Bayhaqiy (04/48) na mtiririko ni wa Ibn Maajah. Ziada ni ya an-Nasaa´iy. Cheni za wapokezi kwa wote ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.

Ya nne: Baadhi ya Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatembelea wagonjwa wa waislamu na wanyonge wao, akisindikiza majeneza yao na wala hakuna mwengine anayewaswalia zaidi yake. Hakika mwanamke mmoja masikini katika watu wa milimani yalirefuka maradhi yake. Kwa hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuulizia kwa yule mwenye kuhudhuria kwake katika majirani zake. Akawaamrisha wasimzike endapo kutazuka chenye kuzuka ili amswalie. Mwanamke huyo akafa kipindi cha usiku na wakaja naye pamoja na wafu wengine – au alisema: “Wakaja naye mahala yanapowekwa majeneza mengine kwenye msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1] – ili Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amswalie mama huyo kama alivyowaamrisha. Wakamkuta Mtume amekwishalala punde tu baada ya swalah ya ´ishaa. Hawakupendeza kumuamsha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka usingizini mwake. Wakamswalia mama huyo kisha wakaondoka naye. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipopambaukiwa na asubuhi akamuulizia kwa yule mwenye kuhudhuria kwake katika majirani zake ambapo wakampa khabari zake na kwamba wao walichukia kumwamrisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ajili yake. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia: “Ni kwa nini mmefanya hivo? Ondokeni!” Wakaondoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka wakasimama karibu na kaburi lake ambapo wakajenga safu nyuma ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama inavyopangwa safu nyuma ya jeneza. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamswalia na akampigia Takbiyr nne kama wanavyopigiwa Takbiyr majeneza mengine.”

Ameipokea al-Bayhaqiy (04/48) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na an-Nasaa´iy (01/280, 281) kwa mukhtasari.

[1] Upande wa mashariki wa msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mahali hapo hii leo ni upande wa mahali wanapoingilia wa kina mama kuanzia kaskazini kwenda mpaka kusini.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 112-115
  • Imechapishwa: 03/08/2020