5- Mdeni ambaye hakuacha mali ambayo inaweza kukidhia deni lake. Mtu huyu anaswaliwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliacha kumswalia mwanzoni mwa Uislamu. Kumepokelewa Hadiyth kadhaa juu ya hilo:

Ya kwanza: “Salamah bin al-Akwaa´ ameeleza:

“Tulikuwa tumekaa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati lilipoletwa jeneza aliswalie wakasema: “Mswalie.” Akasema: “Je, yuko na deni?” Wakasema: “Hapana.” Akasema: “Je, ameacha kitu?” Wakasema: “Hapana.” Akamswalia.”

Kisha wakaleta jeneza lingine wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mswalie!” Akasema: “Je, yuko na deni?” Kukasemwa: “Ndio.” Akasema: “Je, ameacha kitu?” Wakasema: “Dinari tatu. [Akaashiria kwa vidole vyake ´atafanyiwa Kayy´ tatu`.” Akamswalia.”

Halafu akaletewa mtu wa tatu wakasema: “Mswalie!” Akasema: “Je, ameacha kitu?” Wakasema: “Hapana.” Akasema: “Je, analo deni?” Wakasema: “Dinari tatu.” Akasema: “Mswalieni rafiki yenu. Akasema [bwana mmoja katika Answaar anaitwa] Abu Qataadah: “Mswalie, ee Mtume wa Allaah, na juu yangu liko deni lake” ambapo akamswalia.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/367, 369, 374), Ahmad (04/47 na 50) na ziada ni yake. an-Nasaa´iy (01/278) amepokea kutoka kwake kisa cha tatu.

Ya pili: Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza mfano wa kisa cha tatu katika Hadiyth ya Salamah bin al-Akwaa´ na ndani yake imekuja:

“Unaonaje nikimlipia utamswalia?” Akasema: “Ukimlipia kwa ukamilifu nitamswalia.” Abu Qataadah akaenda na akamlipia. Akauliza: “Je, umemlipia kikamilifu anachodaiwa?” Akajibu: “Ndio.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaomba du´aa na akamswalia.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (01/378), at-Tirmidhiy (02/161), ad-Daarimiy (02/263), Ibn Maajah (02/75), Ahmad (05/297, 301, 302, 304, 311) na mtiririko ni wake. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim. Wengine hawakupokea kitendo cha kuondoka kwa Abu Qataadah na kumlipia deni lake kisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamswalia.

Ya tatu: Jaabir amepokea mfano wake na mwishoni mwake ameongeza:

“Wakati Allaah alipomfungulia Mtume Wake akasema: “Mimi ni aula kwa kila muumini kuliko nafsi yake. Hivyo yule atakayeacha deni basi ulipaji wake uko juu yangu na yule atakayeacha mali iko kwa warithi wake.”

Ameipokea Abu Daawuud (02/85), an-Nasaa´iy (01/278) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth hii inayo njia nyingine kupitia kwa Jaabir kwa ziada nyingine ambayo imekwishatangulia katika ukurasa wa 18.

Ya nne: Abu Hurayrah ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiletewa maiti ambaye juu yake anadaiwa ambapo anauliza: “Je, deni lake amelibakishia kitu kitacholilipa?” Mambo yakiwa ni hivo kwamba ameacha ulipaji anamswalia. Vinginevyo hafanyi hivo na anasema: “Mswalieni rafiki yenu.” Wakati Allaah alimpomfungulia funguzi mbalimbali alikuwa akisema: “Hakika mimi ni aula zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao [duniani na Aakhirah. Someni mkitaka:

النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ

“Nabii ni aula zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao.”[1]

Yeyote atakeyefishwa na juu yako analo deni [na hakuacha cha kulipa] basi ulipaji wake uko juu yangu na yeyote aliyeacha mali basi ni kwa warithi wake.”

Ameipokea al-Bukhaariy (04/376 – 09/425), Muslim (05/62), an-Nasaa´iy (01/379) na mtiririko ni wa Muslim. Ziada mbili ni za al-Bukhaariy na Ahmad anayo ya kwanza katika hizo mbili.

at-Tirmidhiy (03/178) ametoa katika ambayo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akayasahihisha, ad-Daarimiy (02/263), at-Twayaalisiy (2524), Ahmad (02/287, 318, 334, 335, 356, 399, 450, 464, 527) amepokea mfano wake. Ni upokezi wa Muslim na vilevile al-Bukhaariy kwa matamshi ambayo yanakaribiana (08/420, 12/07, 22, 40) kupitia njia nyingi kutoka kwa Abu Hurayrah.

Amesema Abul-Bashar Yuunus bin Habiyb, ambaye ndiye mpokezi wa “Musnad” ya at-Twayaalisiy, baada ya hiyo Hadiyth:

“Nimemsikia Abul-Waliyd – akikusudia at-Twayaalisiy – akisema:

“Kwa njia hiyo ndivo amezifanyia kopi zile Hadiyth ambazo zimepokelewa kwa yule ambaye juu yake kuna deni.”

[1] 33:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 110-112
  • Imechapishwa: 03/08/2020