Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Mfano mwingine katika hayo ni alama za Saa, kama kutoka kwa ad-Dajjaal, kuteremka kwa ´Iysaa mwana wa Maryam (´alayhis-Salaam) na kumuua, kujitokeza kwa Ya´juuj na Ma´juuj, kutoka kwa mnyama, jua kuchomoza kutoka magharibi na yanayofanana na hayo katika [maelezo] yaliyosihi upokezi wake.

MAELEZO

3 – Alama za Saa. Makusudio ya Saa ni Qiyaamah. Alama za Saa ni zile alama za Qiyaamah zinazofahamisha kukaribia kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا

“Je, basi wanangojea nini isipokuwa Saa iwafikie ghafla? Na kwa hakika zimekwishakuja alama zake.”[1]

Mtunzi wa kitabu ametaja kuhusu alama za Qiyaamah zifuatazo:

1 – Kujitokeza kwa ad-Dajjaal. Kilugha ni tamko la kupitiliza katika uwongo. ad-Dajjaal ki-Shari´ah maana yake ni mtu mwenye chongo ambaye atajitokeza katika zama za mwisho ambaye atadai uungu. Kujitokeza kwake kumethibiti kwa Sunnah na maafikiano. Mtume (Swala Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Semeni:

قولوا اللهم إني أعوذ بك من عذاب جهنم وأعوذ بك من عذاب القبر وأعوذ بك من فتنة المسيح الدجال وأعوذ بك من فتنة المحيا والممات

“Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba ulinzi kutokamana na adhabu ya Moto, nakuomba ulinzi kutokamana na adhabu ya kaburi, nakuomba ulinzi kutokamana na fitina za al-Masiyh ad-Dajjaal, nakuomba ulinzi kutokamana na fitina za uhai na kifo.”[2]

Ameipokea Muslim.

Mtume (Swala Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba ulinzi kutokamana na mambo hayo ndani ya swalah[3]. Kuna maafikiano juu yake.

Waislamu wameafikiana juu ya kutoka kwake.

Kisa chake ni kuwa atatoka kupitia njia kati ya Shaam na ´Iraaq ambapo awaite watu wamwabudu. Wengi watakaomfuata ni mayahudi, wanawake na watu wa mashambani. Watamfuata vilevile mayahudi 70.000 katika kabila la Aswfahaan. ad-Dajjaal ataenea ulimwenguni kote kama mvua iliyopeperushwa na upepo isipokuwa mji wa Makkah na Madiynah atazuiliwa kuingia. Atakaa kwa muda wa siku arobaini; siku ya kwanza itakuwa kama mwaka, siku ya pili itakuwa kama mwezi, siku ya tatu itakuwa kama wiki na siku zilizosalia zitakuwa kama ilivyozoeleka. Ni mwenye chongo na kati ya macho yake mawili kumeandikwa (ك ف ر). Maandiko hayo yatasomwa na muumini peke yake. Atakuwa na mtihani mkubwa ikiwa ni pamoja na kuziamrisha mbingu mvua inyeshe na ardhi kuchipua mazao. Aidha atakuwa na pepo na moto. Pepo yake ndio moto na moto wake ndio pepo. Mtume (Swala Allaahu ´alayhi wa sallam) amemtahadharisha na akasema:

“Atakayesikia kuhusu ad-Dajjaal basi ajitenge mbali naye na yule atakayekutana naye, basi amsomee mwanzoni mwa Suurah al-Kafh au mwanzoni mwa Suurah al-Kahf.”[4]

[1] 47:18

[2] Muslim (590, 134).

[3] al-Bukhaariy (832) na Muslim (589, 129).

[4] Muslim (2937, 110, 111).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 09/11/2022