2 – Malaika wa mauti kumwendea Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Malaika wa kifo alimwendea Mtume wa Allaah Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa katika umbo la mwanadamu kwa ajili ya kuchukua roho yake ambapo Muusa akampiga ngumi na jicho lake likatoka. Malaika yule akarudi kwa Allaah na kumwambia kuwa amemtuma kwa mja asiyetaka kufa. Allaah akamrudishia jicho lake na kumwambia arudi kwake na aweke mkono wake juu ya mgongo wa fahali[1] na atapata mwaka kwa kila unywele uliyoguswa na mkono wake. Muusa akauliza kitachotokea baada ya hapo ambapo akajibiwa kuwa ni kifo. Akamuomba Allaah amkurubishe katika ardhi takatifu kama kutupa kwa jiwe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Iwapo ningekuweko hapo basi ningekuonyesheni kaburi lake karibu na njia ya al-Kathiyb al-Ahmar. Hadiyth hii imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim.

Mtunzi wa kitabu ameithibitisha katika ´Aqiydah kwa sababu wapo baadhi ya wazushi walioipinga kwa kutumia sababu kwamba haiwezekani kwa Muusa akampiga ngumi Malaika. Tunawaraddi kwamba Malaika alimjia Muusa katika umbo la mtu ambapo Muusa hajui ni nani. Mtu yule anamuomba amtoe nafsi yake. Maumbile ya mwanadamu yanapelekea mtu kujitetea yule anayeombwa nafsi yake. Kama Muusa angelijua kuwa ni Malaika basi asingempiga ngumi. Kwa ajili hiyo mara ya pili alijisalimisha wakati alipokuja katika hali ya kile kinachojulisha kuwa ametoka kwa Allaah ambapo ni kupewa muda wa miaka kadhaa kwa kiasi cha zile nywele za fahali zilizo chini ya mkono wake.

[1] al-Bukhaariy (3407) na Muslim (2372, 157).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 103
  • Imechapishwa: 09/11/2022