Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Ni ni wajibu kuamini yote aliyoelezea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yakasihi kupokelewa kutoka kwake, ni mamoja tuliyoyashuhudia au yaliyofichikana kwetu. Tunajua ya kwamba ni ya haki na ya kweli, ni mamoja vilevile tuwe tumeyafahamu akilini mwetu au tusiyajue na wala hatukagui uhakika wa maana yake. Kwa mfano Hadiyth ya Israa´ na Mi´raaj[1]. Hili lilipitika katika hali ya kuwa macho na haikuwa ndoto. Quraysh wamepinga hilo na wakafanya kiburi kuyakubali – na hawakupinga ndoto.

Mfano mwingine ni Malaika wa mauti alipokuja kwa Muusa (´alayhis-Salaam) ili kuchukua roho yake. Akampiga ngumi na jicho lake likatoka. Akarejea kwa Mola Wake ambapo akamrudishia jicho lake.

MAELEZO

(السمعيات) ni kila kilichothibiti kwa kusikia kwa njia ya Shari´ah na akili ikawa haina nafasi. Kila khabari iliyothibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni lazima kuisadikisha. Ni mamoja tumeishuhudia kwa hisia zetu au imefichikana kwetu. Ni mamoja vilevile tumeidiriki kwa akili zetu au hatukuidiriki. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ۖ وَلَا تُسْأَلُ عَنْ أَصْحَابِ الْجَحِيمِ

“Hakika Tumekutuma kwa haki ukiwa hali ya kuwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwonyaji wala hutoulizwa kuhusu watu wa moto uwakao vikali.”[2]

Mtunzi wa kitabu ametaja miongoni mwa mambo hayo yafuatayo:

1 – Israa´ na Mi´raaj

Israa´ kilugha ni kumsafirisha mtu wakati wa usiku.

Israa´ maana yake katika Shari´ah ni Jibriyl kumsafirisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokea Makkah kwenda Yerusalemu. Amesema (Ta´ala):

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa.”[3]

Mi´raaj kilugha ni kile chombo anachopanda nacho mtu kwa juu.

Mi´raaj ni ngazi ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliipanda kutoka ardhini kwenda juu mbinguni. Amesema (Ta´ala):

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ

“Naapa kwa nyota zinapotua. Hakupotoka swahibu wenu na wala hakukosea.”[4]

mpaka aliposema:

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ

“Hakika aliona miongoni mwa alama za Mola wake kubwa kabisa.”[5]

Kikosi cha wanazuoni wengi wanaona hayo yalifanyika katika usiku mmoja. Wanazuoni wametofautiana ni wakati gani kulitokea tukio hilo. Imepokewa kwa cheni ya wapokezi iliokatika kutoka kwa Ibn ´Abbaas na Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhum) ya kwamba ilikuwa ni katika usiku wa jumatatu tarehe 12 Rabiy´ al-Awwal. Hakuanisha mwaka. Haya ameyapokea Ibn Abiy Shaybah.

Imepokewa kutoka kwa az-Zuhriy na ´Urwah kwamba ilikuwa mwaka mmoja kabla ya kuhajiri. Ameyapokea hayo al-Bayhaqiy. Inakuwa katika Rabiy´ al-Awwal na hakuanisha usiku. Ameyasema hayo Ibn Sa´d na wengineo na an-Nawawiy ameyatilia nguvu. Imepokewa kutoka kwa as-Suddiy kwamba ilikuwa miezi kumi na sita. Ameyapokea hayo al-Haakim. Hivyo inakuwa katika Dhul-Qa´dah. Kuna maoni yanayosema miaka mitatu kabla ya kuhajiri. Maoni mengine yanasema miaka mitano kabla ya kuhajiri. Maoni mengine yanasema miaka sita kabla ya kuhajiri.

Ilikuwa katika hali ya kuwa macho na si usingizini. Quraysh walilikuza na wakalipinga. Ingelikuwa ni katika hali ya usingizi basi wasingelikemea. Kwa sababu hawakupinga jambo la ndoto. Kisa chake ni kuwa Allaah alimwamrisha Jibriyl amsafirishe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa usiku kwenda Yerusalemu akiwa juu ya al-Buraaq kisha akampandisha juu mbinguni mbingu baada ya mbingu mpaka akafika maeneo ambayo alisikia kalamu zikiandika ambapo Allaah akamfaradhishia vipindi vitano vya swalah, akaona Pepo na Moto na akawasiliana na Manabii watukufu. Akawaswalisha akiwa imamu kisha akarudi Makkah na akawaeleza watu yale aliyoyaona ambapo makafiri wakamkadhibisha, waumini wakamsadikisha na wengine wakamtilia mashaka.

[1] al-Bukhaariy (3207, 3887) na Muslim (164, 264).

[2] 02:119

[3] 17:01

[4] 53:01-02

[5] 53:18

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 99-103
  • Imechapishwa: 09/11/2022