Allaah (Ta´ala) amesema:

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” 02:155-156

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ

“Atakayevuta subira na akasamehe, hakika hayo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa.” 42:43

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ

”Bila ya shaka Tutakujaribuni mpaka tutambue wale wenye kupambana na kufanya bidii miongoni mwenu na wenye kuvuta subira na Tutazijaribu habari zenu [kuona ukweli wake zilivyo].” 47:31

Mlango huu ni mpana sana katika Aayah na Hadiyth. Tutataja tu yale yenye kumuamsha mwenye kulala na kumzindua aliyeghafilika. Hadiyth ya Umm Salamah kwa Imaam Ahmad, Muslim na wengine imeshapokelewa kwa njia mbalimbali.

Abu Maalik al-Haarith bin ´Aaswim al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Twahara ni nusu ya imani. [Kusema] “al-Hamdulillaah” kunaijaza mizani. [Kusema] “Subhaan Allaah wal-Hamdulillaah” kunajaza yaliyo baina ya mbingu na ardhi. Swalah ni nuru. Swadaqah ni dalili. Subira ni mwanga. Qur-aan ima ni hoja kwako au dhidi yako.”

Ameipokea Muslim.

Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuna watu katika Answaar walimuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vitu. Akawapa mpaka vikaisha. Baada ya kutoa kila kitu kwa mkono wake akasema:

“Sintokuwa mimi na mali kisha niwabanie. Yule mwenye kujisitiri basi Allaah atamsitiri. Mwenye kutafuta utajiri basi Allaah atamtajirisha. Mwenye kutafuta subira Allaah atamsubirisha. Hakuna yeyote aliyepewa zawadi iliyo bora kama subira.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Swuhayb bin Sinaan (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ajabu iliyoje kwa muumini. Hakika hali yake yote ni kheri na hilo haliwi kwa yeyote isipokuwa kwa muumini tu. Anapofikwa na kitu kizuri, anashukuru na inakuwa ni kheri kwake. Anapofikwa na dhara, anasubiri na inakuwa ni kheri kwake.”

Ameipokea Muslim.

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (´Azza wa Jall) amesema: “Ninapompa mtihani mja wangu kwa vipenzi vyake viwili na akasubiri, basi humpa badala yake Pepo.”

Bi maana macho yake. Ameipokea al-Bukhaariy.

´Atwaa´ bin Abiy Rabaah amesema:

“Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alinambia: “Nisikuonyeshe mwanamke miongoni mwa wanawake wa Peponi?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “Mwanamke huyu mweusi.” Alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Mimi nina kifafa na hubaki wazi. Niombee kwa Allaah (Ta´ala).” Akamwambia: “Ukitaka subiri na utapata Pepo na kama unataka naweza kukuombea kwa Allaah akuponye.” Akasema: “Nitasubiri.” Kisha akasema: “Lakini nabaki wazi. Niombee kwa Allaah nisibaki wazi.” Akamuombea kwa Allaah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muislamu hapatwi na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule Allaah anayemtakia kheri humpa mtihani.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Imesihi ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aligawa mali ambapo baadhi ya watu wakasema:

“Mgawanyo huu haukufanywa kwa ajili ya Allaah.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Allaah amrehemu ndugu yangu Muusa. Hakika aliudhiwa zaidi ya hivi akasubiri.”

Sa´iyd bin Jubayr amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

”Enyi mlioamini! Tafuteni msaada kwa subira na swalah! Hakika Allaah yuko pamoja na wanaosubiri.” 02:153

“Hakuna Ummah uliyopewa subira kama huu. Hukusikia maneno ya Ya´quub (´alayhis-Salaam):

وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ

“Macho yake yakageuka meupe [kwa kulia] kutokana na huzuni.” (12:84)

Sa´iyd bin Mansuur amepokea katika “as-Sunan” yake ya kwamba Ibn ´Abbaas alikuwa nje amesafiri pindi alipopata khabari ya kwamba nduguye Qathm amefariki. Akasema “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea.” Kisha akateremka kwenye mpando wake na akamwacha ngamia atembee kwa miguu yake. Kisha akaswali Rakaa´ mbili na akarefusha Tashahhud. Halafu akasimama na kupanda kwenye kipando chake hali ya kusema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

”Enyi mlioamini! Tafuteni msaada kwa subira na swalah! Hakika Allaah yuko pamoja na wanaosubiri.” 02:153

Ibn Jurayj amesema kuhusu maneno ya Allaah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

”Enyi mlioamini! Tafuteni msaada kwa subira na swalah! Hakika Allaah yuko pamoja na wanaosubiri.” 02:153

“Hivyo viwili vinasaidia katika kufikia huruma wa Allaah.”

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Niliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye alikuwa na homa kali. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Homa yako ni kali.” Akasema: “Ndio. Mimi huumwa homa kali kama wanavyoumwa homa wanaume wenu wawili.” Nikasema: “Ndio maana unalipwa mara mbili.” Akasema: “Ndio. Ndio sababu. Hakuna muislamu yeyote anayechomwa na mwiba isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kama jinsi mti unavyopukucha majani yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

at-Tirmidhiy amepokea ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ujira mkubwa unatokamana na majaribio makubwa. Allaah akiwapenda watu basi huwapa mtihani. Anayeridhia, hupata radhi Zake, na anayekasirika, hupata hasira zake.”

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 135-138
  • Imechapishwa: 30/10/2016