59. Tofauti ya Saudi Arabia na nchi nyigni zinazosemekena ni za Kiislamu

Napendezwa sana na kisa cha mmoja wa watu wema, naye ni Shaykh Thaaniy al-Mansuur (Rahimahu Allaah) kutoka mji wa al-Jubayl katika mkoa wa mashariki mwa Saudi Arabia. Nilikisikia kutoka kwa aliyekisikia moja kwa moja kutoka kwake na mukhtaswari wake ni huu:

”Aliwahi kuitembelea nchi moja ambayo baadhi ya watu wake wamepatwa na fitina ya kujenga juu ya makaburi na kuchupa mipaka kwa watu wake. Akiwa huko alikutana na kundi la watu ndani ya msikiti mmoja uliokuwa na kaburi. Wakamsema yeye na watu wa nchi yake kuwa hawampendi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akawajibu na kuwauliza: “Je, katika nchi yenu kuna baa za pombe na maeneo ya uasherati na ufuska?” Wakasema: “Ndiyo, yapo mengi!” Akasema: “Nchini mwetu hakuna hata sehemu moja kama hiyo.” Kisha akawaambia: “Nini hukumu ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika swalah kwenu?” Wakasema: “Inapendeza.” Akasema: “Kwetu sisi ni nguzo ya swalah; mswaliji asipoisoma basi swalah yake haisihi.” Kisha akauliza: “Basi nani anayestahiki zaidi kuonekana kuwa anampenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?”

Kile alichokisema (Rahimahu Allaah) kinaeleweka wazi katika suala la kwanza. Ama kuhusu suala la pili maoni yanayosema kuwa inapendeza ndio maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni, kama ilivyotangulia huko mbele. Hata hivyo alichokisema hakina tatizo, kwani kilikuwa katika muktadha wa kujadiliana na kujibu hoja za wale waliowasema Ahl-us-Sunnah wa nchi hii kwa madai ambayo hawahusiki nayo kabisa – hawana hatia nayo kama vile jua lisivyoguswa.

Mimi naongeza juu ya alichosema kwamba mahakimu katika nchi hii (Saudi Arabia) wanatoa hukumu kwa mujibu wa Shari´ah ya Kiislamu Tukufu. Ama nchi ile aliyotembelea na nyingine nyingi, basi mahakimu wake wanahukumu kwa mujibu wa sheria za kibinadamu zilizotungwa. Pia katika nchi hii kuna vyuo vingi vinavyoitwa ”Chuo cha Shari´ah ya Kiislamu” (كلية الشريعة) na wahitimu wake huchaguliwa kuwa mahakimu. Ama nchi nyingine nyingi, hata kama kuna kitu cha namna hiyo, basi hupewa jina la ”Chuo cha Shari´ah ya Kiislamu na sheria ya kidunia” (كلية الشريعة والقانون), jina ambalo ni sawa na kusema: “Chuo cha haki na batili.”

Mwaka 1397 nilitembelea Pakistan na kundi la mawakili waliniita kutoa kalima. Nikawashauri watafute kazi nyingine halali na nzuri tofauti na kazi ya uwakili katika mahakama zisizo za Kiislamu. Pia nilimtembelea Rais Zia-ul-Haqq (Rahimahu Allaah) na nikamshukuru kwa juhudi alizokuwa akizifanya katika kutekeleza Shari´ah ya Kiislamu. Miongoni mwa maneno niliyomwambia ni: “Tofauti kati ya Shari´ah ya Kiislamu na sheria za kidunia zilizotungwa na wanadamu ni sawa na tofauti kati ya Allaah na viumbe Wake, kwani Shari´ah ni wahy kutoka kwa Allaah, ilihali sheria hizo ni matokeo ya vichwa vya viumbe wa Allaah.”

Namuomba Allaah (´Azza wa Jall) awawezeshe waislamu kuhukumu kwa Shari´ah ya Mola wao ili wapate furaha ya dunia na Aakhirah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

“Je, wanataka hukumu za kipindi cha kijahili? Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini.”[1]

Amesema kuhusiana na watu wa Kitabu:

وَلَوْ أَنَّهُمْ أَقَامُوا التَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِم مِّن رَّبِّهِمْ لَأَكَلُوا مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِم

“Lau kama wangeliishika vilivyo Tawraat na Injiyl na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, bila shaka wangelikula kutoka juu yao na kutoka chini ya miguu yao.”[2]

 فَمَن تَبِعَ هُدَايَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

”Yeyote atakayefuata uongofu Wangu hakutokuwa na khofu juu yao wala hawatohuzunika.”[3]

فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ

”Atakayefuata uongofu Wangu hatopotea na wala hatopata mashaka. Atakayepuuza ukumbusho Wangu, basi hakika atapata maisha ya dhiki na tutamfufua siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu.”[4]

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi wengine – ni machache mnayoyakumbuka.”[5]

[1] 05:50

[2] 05:66

[3] 02:38

[4] 20:163-164

[5] 07:03

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 83-86
  • Imechapishwa: 01/07/2026