58. Nguzo ya kumi na tatu ya swalah ni kumswalia Mtume katika Tashahhud

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

اللهم صل على محمد و على آل محمد كما صليت على إبراهيم و على آل إبراهيم، إنك حميد مجيد

”Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu. Kama alivyosema al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kutoka kwa Abul-´Aaliyah aliyesema:

“Allaah kumswalia mja Wake ni kule kumsifu katika ulimwengu wa juu.”

Imesemekana vilevile kwamba ni rehema, lakini ya kwanza ndio sahihi zaidi.

Ama kuhusiana na kwamba Malaika pia wanafanya hivyo, maana yake ni kwamba wanamwombea msamaha, na kwamba wanaadamu wanafanya hivyo, maana yake ni du´aa.

MAELEZO

Nguzo ya kumi na tatu katika nguzo za swalah ni kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Namna bora zaidi ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ile inayojulikana kama swala ya Ibraahiym ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafundisha Maswahabah wake walipomuuliza kuhusu namna ya kumswalia. Swalah hii imepokewa kwa matamshi mbalimbali kutoka kwa makundi ya Maswahabah, lakini iliyo bora zaidi ni ile ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliikusanya kati ya kumwombea rehema yeye pamoja na watu wa nyumbani kwake, na kumwombea rehema Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na watu wa nyumbani kwake. al-Bukhaariy (3370) amepokea katika ”as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa ambaye ameeleza:

”Ka’b bin ‘Ujrah alikutana nami ambapo akanambia: “Je, nikupatie zawadi niliyoisikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndiyo, nipatie.” Akasema: “Tulimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Ee Mtume wa Allaah! Vipi tukuswalieni enyi watu wa Nyumba? Hakika Allaah ametufundisha namna ya kukusalimieni.” Akasema: “Semeni:

اللهم صلّ على محمد وعلى آل محمد كما صليت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد، اللهم بارك على محمد وعلى آل محمد كما باركت على إبراهيم وعلى آل إبراهيم إنك حميد مجيد

“Ee Allaah! Msifu Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyomsifu Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa. Ee Allaah! Mbariki Muhammad, jamaa zake Muhammad kama Ulivyombariki Ibraahiym na jamaa zake Ibraahiym. Kwani hakika Wewe ni Mwenye kuhidimiwa na Mwenye kutukuzwa.”

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumsalimu kwa salamu.”[1]

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walijifunza kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) namna ya kumsalimia katika Tashahhud ambayo aliwafundisha ambapo ndani yake imekuja:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Hivyo wakamuuliza kuhusu namna ya kumswali ambapo akawajibu kwa swalah ya Ibraahiym. Ibn Kathiyr amesema katika tafsiri ya Aayah hii: “Maana ya maneno yao: ”Ama kukutolea salamu tumeshajua” ni salamu iliyomo katika Tashahhud aliyo kuwa akiwafundisha kama alivyokuwa akiwafundisha Suurah kutoka ndani ya Qur-aan ambayo ndnai yake imekuja:

السلام عليك أيها النبي ورحمة الله وبركاته

”Amani iwe juu yako, ee Mtume, rehema na baraka za Allaah.”

Imekuja katika ”Musnad” ya Imaam Ahmad (17072), ”al-Mustadrak” ya al-Haakim (1/268) ambaye amesema: “Hadiyth hii ni Swahiyh kwa mujibu wa masharti ya Muslim” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye kupitia kwa Abu Mas’uud al-Answariy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

”Mtu mmoja alikuja na kuketi mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na sisi tulikuwa pamoja naye ambapo akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Ama salamu juu yako tumeshajua. Basi vipi tukuswalie wakati tunaposwali ndani ya swalah zetu swalah akuswalie… ?”

Katika mlolongo wa wapokezi kwa Ahmad na al-Haakim yupo Muhammad bin Ishaaq ambaye ni mwenye kufanya hadaa, lakini ametamka kwa uwazi kuwa amesimuliwa kwake kutoka kwa Muhammad bin Ibraahiym at-Taymiy ambapo akasema:

“Muhammad bin Ibraahiym bin al-Haarith at-Taymiy amenisimulia kuhusu kumswalia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati muislamu anapomswalia ndani ya swalah yake.”

Ndani ya haya kuna dalili kwamba swalah na salamu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vinakusanywa katika sehemu ya mwisho ya swalah. Ibn Kathiyr amenukuu katika tafsiri yake maoni ya uwajibu wa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya Tashahhud ya mwisho, kutoka kwa Imaam ash-Shaafi’iy, Imaam Ahmad na Ishaaq bin Raahawayh. Hadiyth ya Abu Mas’uud (Radhiya Allaahu ´anh) iliyotangulia pia inafahamisha juu ya hilo, kama alivyoeleza Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah). Hata hivyo kikosi kikubwa cha wanazuoni wanaona kuwa sio jambo la wajibu.

[1] 33:56

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 80-83
  • Imechapishwa: 01/07/2026