1 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee ´Amr! Uzuri wa pesa ni kwa yule mtu ambaye ni mwema!”

2 – Katika khabari hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaweka wazi kwamba inafaa kukusanya pesa kwa njia ya kwamba ni wajibu na halali yule anayetekeleza haki ya pesa hizo. Hapana shaka kwamba mali nzuri imetajwa sambamba na mtu mwema. Kwa sababu si venginevo inafaa kukusanya mali ambayo sio haramu kwa mtu huyo. Baada ya hapo mtu huyo anatakiwa kutekeleza haki ya Allaah kwa pesa hizo.

3 – Qays bin ´Aaswim alisema kuwaambia wanae wakati alipokuwa anataka kukata roho:

“Kuweni na tafuteni pesa! Inajulisha mkarimu. Ambaye anazo pesa hahitaji kusimangwa. Nakutahadharisheni kuwaombaomba watu! Kwani kuombaomba ndio pato la mwisho la mtu.”

4 – Miongoni mwa mambo bora yanayomnufaisha mtu duniani na Aakhirah ni kumcha Allaah na matendo mema.

5 – Ni wajibu kwa mtu mwenye busara afanye kazi katika ujana wake kwa ajili ya kukamilisha mahitaji yake, kama kitu ambacho kamwe hakitomwacha, kuitengeneza dini yake, kama kitu ambacho hatokipata hiyo kesho. Msimamo wake wa pesa uwe kwa ajili ya kuweza kuishi, kuilinda nafsi yake, kunufaika nayo huko Aakhirah na kumridhisha Muumba wake. Umasikini ni bora kuliko kutajirika kwa njia ya haramu. Tajiri na mtu asiyestahili ni mbaya zaidi kuliko mbwa.

6 – Muhammad bin al-Munkadir amesema:

“Utajiri ni msaada mzuri wa kuweza kumcha Allaah.”

7 – az-Zubayriy amesema:

“´Umar bin al-Khattwaab alipita pambizoni mwa Muhammad bin Maslamah ambaye alikuwa anapanda mitende midogo. Akasema: “Unafanya nini, ee Ibn Maslamah?” Akasema: “Unaona. Nafanya hivo ili nijitosheleze na watu.”

8 – ´Abdaan amesema:

“Niliingia kwa ´Abdullaah bin al-Mubaarak ambaye alikuwa ameketi na kulia. Nikasema: “Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Kwa nini unalia?” Akasema: “Nimepoteza bidhaa yangu.” Nikasema: “Unalia kwa sababu ya pesa?” Akajibu: “Ndio inayosimamisha dini yangu.”

9 – Hakika miongoni mwa watu walio na furaha zaidi ni yule mwenye kujizuia wakati anapokuwa tajiri na mwenye kukinaika anapokuwa masikini. Umasikini unaondosha akili na muruwa. Unaondosha elimu na adabu. Umasikini unakaribia kuwa ukafiri. Masikini daima ni mwenye kujengewa dhana mbaya. Anakusanyikiwa na mabalaa yote. Isipokuwa yule masikini ambaye amejaaliwa moyo wenye uchaji na wenye kukinaika.

10 – Ayyuub amesema:

“Abu Qilaabah alinambia: “Ee Ayyuub! Lazimiana na soko lako. Hutoacha kuwa ni mwenye kuheshimika kwa ndugu zako muda wa kuwa si mwenye kuwahitaji.”

11 – Hakuna sifa inayosemwa vizuri kwa tajiri isipokuwa kwa masikini inakuwa yenye kusemwa vibaya. Masikini akiwa mvumilivu, kunasemwa kuwa ni mpumbavu. Masikini akiwa mwenye busara, basi kunasemwa mjanja. Maskini akiwa mfasaha, basi kunasemwa anabwabwaja. Masikini akiwa na akili, basi kunasemwa kuwa ni mkali. Masikini akinyamaza kimya, basi kunasemwa kuwa ni mjinga. Masikini akiwa mwangalifu, basi kunasemwa kuwa ni mwoga. Masikini akiwa mjuzi, basi kunasemwa kuwa ni mwenye ujasiri wa kipumbavu. Masikini akiwa mkarimu, basi kunasemwa kuwa ni mwenye kufanya israfu. Masikini akiwa mwenye kuhifadhi, basi kunasemwa kuwa ni mwenye choyo.

12 – Pesa mbaya kabisa ni ile ambayo imechumwa kwa njia ya haramu na imetumika kwa njia ambayo ni haramu. Uwepo wa pesa na kutokuwepo kwake hakutokani na subira na njia. Kunatokana na mgao na neema za Muumbaji.

13 – Ka´b amesema:

“Mtu wa kwanza kutengeneza dinari na dirhamu alikuwa ni Aadam (´alayhis-Salaam). Akasema: “Haiwezekani kuishi bila viwili hivi.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 223-229
  • Imechapishwa: 28/08/2021