59. Mfungaji anatakiwa kujiepusha na nyimbo na muziki

Mfungaji anatakiwa kujiepusha na ala za pumbao na muziki kwa aina zake zote. Ni vitu vya haramu. Uharamu na dhambi inakuwa kubwa zaidi vikiambatana na nyimbo kwa sauti nzuri na nyimbo zinazochochea. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ

“Miongoni mwa watu wako ambao hununua maneno ya upuuzi ili wapoteze kutokamana na njia ya Allaah pasi na elimu na huichukulia mzaha – hao watapata adhabu ya kutweza.”[1]

Imesihi kutoka kwa Ibn Mas´uud kwamba aliulizwa juu ya Aayah hii ambapo akasema:

“Naapa kwa Yule ambaye hapana mungu wa haki mwingine zaidi Yake kwamba ni nyimbo.”

Imesihi pia kutoka kwa Ibn ´Abbaas na Ibn ´Umar na ametaja Ibn Kathiyr kutoka kwa Jaabir, ´Ikrimah, Sa´iyd bin Jubayr na Mujaahid. al-Hasan amesema:

“Aayah hii imeteremka juu ya nyimbo na firimbi.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha kutokamana na ala za nyimbo na akaziambatanisha na uzinzi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika watakuweko katika Ummah wangu watu wataohalalisha uzinzi, hariri, pombe na zana za muziki.”

Amepokea al-Bukhaariy.

Maana ya ´watahalalisha` watayafanya hali ya wenye kuhalalisha bila ya kujali, mambo ambayo yametokea katika wakati wetu huu. Utawaona watu wenye kutumia zana hizi za muziki au wanazikiliza kana kwamba ni kitu cha halali. Jambo hili ni miongoni mwa mambo ambayo wamefaulu kwayo maadui wa Uislamu dhidi ya vitimbi yao juu ya waislamu mpaka wakawazuia kutokamana na utajo wa Allaah na mambo yenye umuhimu nao katika dini na dunia yao. Hali imefikia kiasi cha kwamba wengi wao wamekuwa ni wenye kuisikiliza zaidi kuliko wanavosikiliza kisomo cha Qur-aan, Hadiyth na maneno ya wanazuoni ambayo ndani yake kuna ubainifu wa hukumu za Shari´ah na hekima zake.

Enyi waislamu! Jichungeni na mambo yanayoiharibu na kuipunguza swawm. Ilindeni pia na maneno ya uongo na kuyatendea kazi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”

Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ukifunga basi yafunge pia masikizi yako, macho yako na ulimi wako dhidi ya uongo na mambo ya haramu. Usiwaudhi majirani. Uwe na upole na utulivu. Siku ya kufunga na kula kwenu visilingane.”

[1] 31:06

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 71
  • Imechapishwa: 23/04/2021