34. Hali tatu ambazo vifunguzi vinamfunguza mfungaji

Swali 34: Nikimuona mfungaji anakula na kunywa mchana wa Ramadhaan kwa kusahau akumbushwe au hapana?

Jibu: Mwenye kumuona mfungaji anakula au anakunywa mchana wa Ramadhaan basi ni lazima amkumbushe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nikisahau nikumbusheni.”[1]

Mtu mwenye kusahau amesamehewa kwa kusahau kwake. Lakini yule mtu mwenye kukumbuka ambaye anajua kuwa kitendo hichi kinaiharibu funga yake na asimwelekeze anakuwa amefanya upungufu. Huyu ni nduguye na hivyo ni lazima ampendelee kile anachoipendelea nafsi yake mwenyewe.

Kwa kufupisha ni kwamba yule mwenye kumuona mfungaji anakula au anakunywa mchana wa Ramadhaan kwa kusahau ni lazima amkumbushe. Ni lazima kwa mfungaji kujizuia na kula papo hapo na haijuzu kwake kuendelea katika kula au kunywa kwake. Bali ikiwa mdomoni mwake ana maji au kitu katika chakula basi analazimika kukitema. Haijuzu kwake kukimeza baada ya kukumbuka au kukumbushwa kuwa amefunga.

Kupitia mnasaba huu napenda kubainisha kuwa vifunguzi vinavyomfunguza mfungaji havifunguzi isipokuwa katika hali tatu:

1- Akiwa amesahau.

2- Akiwa mjinga.

3- Akiwa si mwenye kukusudia.

Akisahau ambapo akala au kunywa basi funga yake ni kamilifu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kusahau ilihali amefunga ambapo akala na akanywa basi funga yake ni sahihi. Hakika si vyenginevyo Allaah ndiye kamlisha na kumnywesha.”[2]

Akila au akinywa huku akidhani kuwa alfajiri bado haijachomoza au akidhani kuwa jua limekwishazama kisha baadaye ikambainikia kuwa jambo ni kinyume na alivyodhania, basi funga yake ni sahihi. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliopokelewa na al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh” yake ambapo amesimulia:

“Siku moja ya mawingu wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulifuturu. Kisha baadaye jua likachomoza. Hakuwaamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulipa.”[3]

Kulipa ingelikuwa ni lazima basi angeliwaamrisha na wangeliamrishwa basi tungelinakiliwa. Kwa sababu wangeliamrishwa ingekuwa ni katika Shari´ah ya Allaah. Shari´ah ya Allaah ni lazima iwe imehifadhiwa na yenye kufikishwa mpaka siku ya Qiyaamah.

Vivyo hivyo asipokusudia kufanya cha kufunguza hafungui. Kwa mfano wakati yuko anasukutua maji yakaingia tumboni mwake. Hafungui kwa jambo hilo. Hakukusudia. Mfano mwingine akilala akaota ambapo akatokwa na manii funga yake haiharibiki. Kwa sababu amelala na hakukusudia. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ

”Hapana dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea, lakini isipokuwa katika yale yaliyoyakusudia nyoyo zenu.”[4]

[1] al-Bukhaariy (40) na Muslim (572).

[2] Muslim (2686).

[3] al-Bukhaariy (1959).

[4] 33:05

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 30-32
  • Imechapishwa: 24/04/2021