58. Uombezi wa kwanza kuombewa wataosimama kwenye kiwanja

Kuna uombezi aina sita. Kuna uombezi ambao ni maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uombezi mwingine anashirikiana yeye na wengineo katika Malaika, mawalii na waja wema na watoto waliokufa kabla ya kubaleghe.

Uombezi maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni:

1- Uombezi mkubwa. Ni kile cheo chenye kusifika. Ni pale ambapo watu watakuwa wamesimama katika kiwanja cha mkusanyiko na watawaomba Mitume wawaombee mbele ya Allaah awaondoshe katika kisimamo hicho. Kwa sababu watasimama kwa kipindi kirefu pamoja na joto kali, dhiki na kisimamo kirefu ambapo watasimama miaka elfu khamsini. Watasogea mbele na wamtake Aadam (´alayhis-Salaam), ambaye ndiye baba wa watu, awaombee mbele ya Allaah ahukumu kati yao na awapumzishe kutokamana na kisimamo. Aadam ataomba udhuru. Kisha wamtake Nuuh (´alayhis-Salaam), ambaye ndiye Mtume wa kwanza, aombe udhuru. Kisha wamtake Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ambapo ataomba udhuru. Kisha wamtake Muusa (´alayhis-Salaam) ambapo ataomba udhuru. Kisha wamtake ´Iysaa (´alayhis-Salaam) ambapo ataomba udhuru. Kisha wamtake Muhammad (´alayhis-Salaam) ambapo ajiandae kwayo na aseme:

“Mimi ndiye mwenye kuistahiki, mimi ndiye mwenye kuistahiki.”[1]

Hayo yatakuwa baada ya kuiomba kutoka kwa wale Mitume bora wote ambapo waombe udhuru isipokuwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika yeye atakubali kuwaombea mbele ya Allaah. Aporomoke chini hali ya kuwa ni mwenye kusujudu chini ya ´Arshi, amuombe Allaah (´Azza wa Jall) na amsifu. Ataendelea kufanya hivo mpaka pale atapoambiwa:

“Ee Muhammad! Inua kichwa chako, omba utapewa na shufai utasikilizwa.”

Atawaombea waliosimama uwanjani ili apitishe hukumu yake na awapumzishe kutoka katika kisimamo na Allaah akubali uombezi wake. Hichi ndio cheo chenye kusifika ambacho Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema juu yake:

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا

“Amka sehemu ya usiku na uswali ni ziada ya sunnah kwako; bila shaka Mola wako atakuinua cheo kinachosifika.”[2]

Ni cheo ambacho atasifiwa na wa mwanzo na wa mwisho na kitadhihirisha fadhilah na ubora wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kisimamo hichi kitukufu.

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193) kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] 17:79

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 09/04/2021